other blog

Jumatatu, 19 Oktoba 2015

MWADADA NOREEN KAHAYA...EAGLEFM


Msanii wa muziki wa Reggae, Jhikolabwino
Manyika 'Jhikoman' akipiga gitaa mbele ya
waandishi wa habari muda mfupi baada ya
mkutano ulioongelea tamasha la 'Karibu
Music Festival 2015'. Kulia ni Meneja
Uvumbuzi wa Serengeti Breweries
Limited, Attu Mynah. Picha na Said Hamis
Dar. Wadau wa muziki nchini, Afrika
Mashariki na dunia nzima kwa ujumla
watapata fursa kujumuika pamoja na
kubadilishana uzoefu wa kazi zao
katika tamasha la pili la muziki
maarufu kama ‘Karibu Music Festival’
litakalofanyika mapema mwezi ujao
huko Bagamoyo.
Tamasha hilo lenye kauli mbiu ya
‘Fahari ya Tanzania’ linalennga kukuza
muziki wa Kiafrika na kuonesha
tamaduni za Kiafrika kwa dunia nzima
kupitia jukwaa la muziki
litakalokutanisha wanamuziki kutoka
sehemu mbalimbali duniani.
Akizungumza na waandishi wa habarI
leo katika Ukumbi wa Idara ya Habari
Maelezo mwakilishi wa Karibu Music
Festival, Ernest Biseko alisema
Tamasha hilo mwaka huu
litahudhuriwa na wanamuziki
wakubwa akiwemo mkongwe Papa
Wemba, Sarabi Band, H-Art The Band,
Yuzzo & Frontline Band.
Biseko alisema kuwa, wasanii toka
Tanzania ni pamoja na Jhiko Manyika
(Jhikoman) na band yake ya
Afrikabisa, Tomgwa Ensembe, mshindi
wa shindano la vipaji la BSS mwaka
2008, Misoji Nkwambi, Ze Spirit, Isha
Mashauzi, Damian Soul na bandi yake,
Juma Nature, Msafiri Zawose na band
yake.
“Pamoja na kwamba lengo kubwa ni
kukuza muziki wa Kiafrika na
tamaduni zake pia tunataka liwe
tamasha pekee Afrika Mashariki
kukuza uchumi na kuleta maendeleo
kwa watu wake ndio maana biashara
na maenesho ya bidhaa mbali mbali ni
sehemu ya tamasha hili,” alisema
Biseko.
Naye mwakilishi wa wanamuziki
watakaoshiriki katika tamasha hilo,
Jhikolabwino Manyika maarufu kama
Jhikoman ambaye pia ni msanii
maarufu wa miondoko ya Reggae
nchini alisema mashabiki wa muziki
watarajie kuona wasanii wote
wakitumbuzia bila kutumia CD
‘playback’.
Jhikoman alisema kuwa kupitia
tamasha hilo anatarajia kupata nafasi
ya kujifunza kutoka kwa bendi
nyingine jinsi ya kukuza kazi zao na
kudumisha urafiki utakaoleta manufaa
katika kazi yake.
Tamasha hilo litaanza kwa matembezi
kuashiria uzinduzi wake na pia
kutakuwa na mafunzo mbali mbali
yenye mlengo wa kuwasaidia wadau
wa muziki kufahamu mambo mbali
mbali kwenye maswala ya kiutawala
na jinsi ya kujitangaza, mambo ya hati
miliki, ngoma za asili, kupiga ngoma,
na mengineyo.
Kiingilio katika tamasha hilo ni
Sh2,500 kwa watoto, watu wazima
watakaonunua tiketi zao kabla ya
tamasha itakua ni Sh 5,000 na kwa
wale watakaonunua getini itakua Sh
7,000 na kwa watu maalumu (VIP)
tiketi zitauzwa kwa Sh 30,000.

MABERE GODLUCK SPORT EAGLFM..... Messi ajipa matumaini


Mshambuliaji wa Azam, Ramadhan
Singano ‘Messi’
Dar es Salaam. Mshambuliaji wa
Azam, Ramadhan Singano ‘Messi’
amesema kuwa hakatishwi tamaa na
kitendo cha kutopata nafasi kwenye
kikosi cha kwanza cha timu hiyo na
ana uhakika atapata nafasi hiyo ndani
ya kipindi kifupi kijacho.
Singano aliyejiunga na Azam msimu
huu akitokea Simba, amekuwa hana
nafasi kwenye kikosi cha kwanza cha
timu hiyo kutokana na ushindani
mkubwa uliopo kwa washambuliaji
mbalimbali waliosajiliwa na klabu
hiyo.
Miongoni mwa washambuliaji
wanaowania namba naye ni, Kipre
Tchetche, John Bocco, Farid Mussa,
Didier Kavumbagu na Allan Wanga
walioifanya Azam iwe moja ya timu
zenye safu kali ya ushambuliaji
kwenye ligi.
Singano aliliambia gazeti hili jana
kuwa si jambo la kushangaza kwa
mchezaji kutopata nafasi ya kuanza
kwenye kikosi cha kwanza kwani ni
jambo inategemeana na matakwa ya
kocha.
“Mwenyezi Mungu ndiye kila kitu
katika maisha na yeye ndiyo
kampangia kila mwanadamu riziki.
“Nafurahia maisha hapa na ingawa
bado sijapata nafasi ya kucheza
kwenye kikosi cha kwanza mara.
Naendelea kufanya mazoezi na
naamini Mungu atanisaidia kupata
nafasi muda siyo mrefu,” alisema
Singano.

GODLUCK MABERE EAGLEFM ON SPORT...


Mshambuliaji wa Mbeya City, Haruna
Moshi ‘Boban’
Mbeya. Wakati Simba ikiibuka na
ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mbeya
City, imebainika kuwa Wekundu hao
wa Msimbazi waliingia uwanjani
wakiwaza namna ya kumkaba kiungo
wao wa zamani Haruna Moshi ‘Boban’.
Simba waliingia mchezo wakiwaza
Boban angeingia na jipya gani,
baadaye waligundua kiungo huyo
hawatishi kwani ameongeza uzito kiasi
cha kushindwa kuendana na kasi ya
mechi huo uliochezwa Uwanja wa
Sokoine.
Hiyo ilikuwa mechi yake ya kwanza
kwa Boban ya Ligi Kuu Bara msimu
huu baada ya kuchelewa kujiunga na
kikosi hicho na alifanya mazoezi siku
moja kabla ya mechi hiyo na kocha wa
City, Meja Mstaafu Abdul Mingange
kuamua kumtumia.
Wachezaji waliowahi kucheza naye
Boban akiwa Simba, akiwamo kocha
msaidizi, Seleman Matola na nahodha
wa timu hiyo, Musa Hassan ‘Mgosi’
walimwelezea Boban kuwa ni mchezaji
mzuri, ila kwa sasa anahitaji kuongeza
juhudi katika mazoezi kwani
anaonekana kuwa mzito kutokana na
mwili wake kuongezeka uzito.
“Boban nimemwona, ni mchezaji
mzuri, kikubwa anachopaswa
kukifanya kwasasa ni kuongeza
mazoezi, maana amekuwa na mwili
mnene, ila kiuwezo bado anaonekana
yupo fiti na anaweza kukubadilishia
matokeo muda wowote,” alisema
Matola.
Naye Mgosi alisema, “namfahamu
Boban, si mchezaji wa kubezwa
unapocheza naye, anaweza kukuliza
muda wowote, ila kwa sasa bado
hajapata mchezaji ndani ya Mbeya
City ambaye anaweza kumwelewa kwa
haraka uchezaji wa Boban ama nini
anataka anapokuwa uwanjani.
“Boban siyo mchezaji wa
kukimbiakimbia, jinsi anavyocheza
ndivyo hivyo hivyo, anavyoweza
kukufunga bila kutarajia, ila
namshauri aongeze mazoezi apunguze
mwili na atawasaidia Mbeya City kama
watamtumia vizuri,” alisema Mgosi.
Kocha mkuu wa Simba, Dylan Kerr
naye alisema kuwa amepata taarifa za
Boban kuwa ni mchezaji hatari na
anapaswa kuchungwa katika mechi
hiyo japokuwa hajawahi kumuona
akicheza.
“Tunashukuru tumeshinda mechi hii
na kupata pointi tatu, Mbeya City siyo
timu mbaya na wamecheza kwa
kiwango cha juu, ila hawajapata bahati
ya kutufunga.”

GUDLACK MABERE ON SPORT. EAGLEFM... Ubonge ‘nyanya’ wamtesa Boban Wakati Simba ikiibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mbeya City, imebainika kuwa Wekundu hao wa

POSTED BY MABERE GODLUCK EAGLEFM... KATIKA SPORT


Mshambuliaji wa Barcelona, Neymar da
Silva Santos Junior (wa pili kushoto)
akiwania mpira na beki wa Rayo Vallecano
Nacho (kushoto) na kiungo Diego Llorente
wakati wa mchezo wa Ligi Kuu Hispania
uliozikutanisha timu hizo kwenye Uwanja
wa Camp Nou, Barcelona. Barca ilishinda
5-2. Picha na AFP
Madrid, Hispania. Real Madrid na
Barcelona zimeng’ang’ania kileleni
mwa La Liga wakati Cristiano Ronaldo
akiweka rekodi Real ikishinda 3-0 dhidi
ya Levante, huku Neymar akifunga bao
manne wakati Barca ikichapa Rayo
Vallecano 5-2.
Real imeutumia vizuri uwanja wake
Bernabeu, wakati Ronaldo akivunja
rekodi ya Raul akifunga mabao 324
katika misimu yake saba aliyocheza
kwa miamba hiyo ya Hispania.
Barca ilitumia vizuri wenyeji wake,
huku safu yao ya ulinzi ikionyesha
kupwaya na kuhitaji uwezo wa binafsi
wa Neymar kusawazisha kutoka
nyuma kabla ya kuifunga Rayo
iliyocheza soka zuri la kushambulia
kwenye Uwanja Nou Camp.
Miamba hiyo ya Hispania
inayosumbuliwa na majeruhi sasa
zinaongoza ligi zikiwa na pointi18
katika michezo nane, huku Real
ikiongoza kwa tofauti ya mabao.
Villarreal iliyokuwa ikishikiria usukani
kwa muda, imeporomoka hadi nafasi
ya tatu, kabla ya mechi yake ya jana
dhidi ya Celta Vigo, wakati Atletico
Madrid inayoshika nafasi ya tano
itacheza na Real Sociedad.
Marcelo alifunga bao la kwanza la Real
katika dakika 27, wakati alipobadilisha
pasi na Ronaldo na kupiga shuti
lililompata kipa Ruben wa Levante.
Ronaldo alifunga bao la pili dakika tatu
baadaye kwa shuti la mbali lililojaa
wavuni , na kumaliza ukame wake wa
kutokufunga katika michezo minne
iliyopita ya ligi.
Naye Jese akiingia akitokea benchi
aliifunga bao la tatu dakika nane kabla
ya filimbi ya mwisho na kuhakikishi
ushindi 3-0, wakati Real ikijiandaa na
mchezo wa Ligi ya Mabingwa wa
Kundi A dhidi ya Paris St Germain.
Barca yatakata
Barca ilimkosa nyota wake Lionel
Messi na nahodha wake Andres
Iniesta, wakati Javi Guerra alipofunga
bao la kuongoza kwa Rayo katika
dakika15.
Ivan Rakitic na Luis Suarez awali
alishindwa kumfunga Tono wakati
alipokutana uso kwa uso na kipa huyo
wa Rayo, lakini Barcelona ilisawazisha
dakika 22, kupitia Neymar kwa
mkwaju wa penalti.
Mbrazil huyo amechukua jukumu la
kuibeba timu hiyo baada ya
kukosekana kwa Messi, alidondoshwa
tena kwenye eneo la hatari dakika 13
na kufunga penalti yake ya pili.
Neymar alifunga bao la tatu dakika 69
na kupachika la nne dakika 70 kufanya
matokeo kuwa 4-1, magoli hayo
yanamfanya Neymar kuwa mchezaji
mwingine wa Barca mbali ya Messi
kufunga idadi hiyo ya magoli tangu
Samuel Eto’o alivyofanya hivyo 2008.
Neymar alitegeneza bao la tano kwa
kupiga krosi nzuri iliyomaliziwa na
Suarez na kuhitimisha kalamu hiyo ya
mabao 5-2.
Jozabed alitumia vizuri kutumia
udhaifu wa mabeki wa Barca kufunga
bao la pili kwa Rayo katika dakika ya
86.
“Neymar amekuwa katika kiwango
kizuri tangu kuanza kwa msimu huu,”
alisema Luis Enrique. “Wakati
anapoingia katika eneo la hatari
hakuna wa kumzuia.”
Sevilla inayojiandaa kucheza na
Manchester City katika Ligi ya
Mabingwa Jumatano, imelazimishwa
sare 1-1 na Eibar, wakati Valencia
ikipata ushindi mnono wa mabao 3-0
dhidi ya Malaga.

POSTED BY PINDA ..EAGLEFM

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda
Dar es Salaam. Waziri Mkuu Mizengo
Pinda, jana alitumia Ibada ya Shukrani
iliyofanyika katika Parokia ya
Hananasifu, Jimbo Kuu Katoliki la Dar
es Salaam, kumshukuru Mungu kwa
kumwezesha kulitumikia Taifa kwa
zaidi ya miaka 15 na kuwaomba
Watanzania wamsamehe kwa
matamshi aliyoyatoa akiwa kiongozi,
huenda yaliwakwaza baadhi yao.
Pinda ambaye amekuwa Waziri Mkuu
kwa miaka minane na miezi tisa,
Waziri kwa miaka miwili na nusu na
Naibu Waziri kwa miaka mitano,
alisema anasikia fahari kumaliza
uongozi wake kwa furaha na amani.
Moja ya kauli tata zilizowahi kutolewa
na kiongozi huyo iliyozua sintofahamu
ni ile ya Juni 29, 2013 katika ukumbi
wa Bunge mjini Dodoma alipoviagiza
vyombo vya dola kuwashughulikia kwa
kuwapiga wale watakaokataa kutii
amri wakati wakifanya vitendo vya
uvunjifu wa amani.
Kauli nyingine tata ni ile ya mwaka
2009 baada ya kuwaeleza wanaoua
watu wenye ulemavu wa ngozi
(albino) pamoja na vikongwe hawana
budi kuuawa kwa kuwa wakisubiri
mahakama kuwahukumu, watakuwa
wanakosea.
“Katika ibada hii ya shukrani,
nimemuomba Mungu anisamehe kwa
matamshi niliyoyatoa nikiwa kiongozi
yanaweza kuwa yaliwaudhi watu bila
mimi kujua.
“Uwaziri Mkuu ni kazi ngumu yenye
changamoto nyingi. Nitakuwa mtu wa
ajabu nisipomshukuru Mungu kwa
uongozi wake katika kipindi chote
hicho tangu nikiwa naibu waziri hadi
kuteuliwa kuwa Waziri Mkuu,”
alisema.
Pinda alisema katika utumishi wake
kwa umma amejifunza mambo mengi
lakini kikubwa zaidi ni kujua jinsi ya
kuishi na watu.
Katika hatua nyingine, Abate Thadei
Mhagama wa Abasia ya Hanga,
aliwataka waumini nchini wazidishe
maombi kwa kufunga na kuomba kwa
siku sita zilizobaki kabla ya kufanyika
kwa Uchaguzi Mkuu.
“Ninawaomba waumini wote tuzidishe
sala ili nchi iendelee kuwa na amani
na upendo, tumwombe Mungu pia
atuwezeshe kupata viongozi
aliowandaa kwa yeye kwa maana ya
rais, wabunge na madiwani,” alisema
Mhagama.
Alisema uchaguzi wa mwaka huu ni wa
aina yake kwani demokrasia imekuwa
miongoni mwa Watanzania.
“Sote ni mashahidi, tumeona kwenye
mikutano kila mgombea akija sote
tunajaa huko. Hii ni kwa sababu
hatujui yupi ni yupi, ndiyo maana
nasisitiza kuwa tumuombe Mungu
atuletee yule ambaye amemuandaa
yeye,” alisisitiza.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya
Baraza la Walei katika parokia hiyo,
Arbogasti Warioba alisema:
“Sote tunatambua kuwa kazi
aliyoifanya Waziri Mkuu Pinda ilikuwa
ngumu, misafara ilikuwa ni mingi na
wakati mwingine ilikuwa ya mwendo
mkali, lakini Mungu alimtetea na
kumlinda hadi leo yuko salama.
Tunakushukuru pia kwa ushirikiano
ulioendelea kutuonyesha wakati ukiwa
madarakani na tunakuombea uendelee
kuwa na ucha Mungu katika maisha
yako ya uraiani.”

POSTED BY VUMILIA NKYA A.K.A VEN DA CLASSIC....EAGLEFM... Magufuli: Asiyefanya kazi


Mgombea urais wa CCM, Dk John
Magufuli akihutubia mkutano wa kampeni
wilayani Misungwi, Mwanza jana. Picha na
Mpigapicha Wetu
Magu/Misungwi. Mgombea urais wa
CCM, Dk John Magufuli amewataka
wananchi kujipanga kufanya kazi kwa
sababu Serikali yake haitavumilia
watu wavivu.
Akihutubia mkutano wa kampeni
katika Uwanja wa Shule ya Msingi
Misungwi jana, Dk Magufuli alisema
hata vitabu vya dini vimeelekeza
kwamba asiyefanya kazi na asile, hivyo
wanaoahidi vitu vya bure
wanawadanganya Watanzania.
“Tujipange kufanya kazi, hata
maandiko ya vitabu vitakatifu
yanasema, asiyefanya kazi asile…
Misungwi nitaibeba kwa nguvu zangu
zote nikichaguliwa,” alisema.
Pia alisema nyumba za tembe ambazo
zinaahidiwa na wagombea wenzake
kwamba zitaondolewa ndani ya siku
100 ni uongo hivyo wasisikilizwe, bali
atakachofanya ni kuhakikisha bei ya
vifaa vya ujenzi inapungua na
ameanza na saruji.
Alisema anatambua kuwa wilaya hiyo
inakabiliwa na tatizo la maji na
kuwaahidi wananchi kulishughulikia
na wasimsumbue mbunge wao na
kwamba anapoahidi kutoa Sh50
milioni kila kijiji nchini watu
wanamshangaa lakini Serikali ina
fedha, nyingine zilikuwa zinatafunwa
na mafisadi.
“...Ndiyo maana baada ya kusikia
nimetangazwa mengine yakakimbia…
hivi sasa wanasema Serikali haijafanya
chochote wakati wengine wamezeekea
humu mpaka wakang’oka meno na
kuwekewa ya bandia, mbona
hawakuondoka muda wote?” alihoji Dk
Magufuli.
Mgombea huyo huku akichomeka
lugha ya Kisukuma kila mara, alisema
ujenzi wa barabara ya Usagara –
Kisema ukikamilika, malori yatakuwa
hayaruhusiwi kuingia katikati ya mjini
wa Mwanza. Aliahidi kufufua viwanda
vya kuchambua pamba ili kuleta
mabadiliko ya kweli.
Dk Magufuli aliahidi kufufua kilimo
cha pamba kwa kuhakikisha mkulima
anapata pembejeo na kunufaika na zao
hilo na kwamba, haiwezekani pamba
ilimwe Tanzania Ulaya wavae nguo
mpya halafu Watanzania waletewe
mitumba.
Hata hivyo, mgombea huyo akiendelea
kutoa ahadi sauti za wanawake
zilisikika zikimtaka kuzungumzia
samaki kazi ambayo ndiyo
wanayoitegemea kiuchumi, hivyo
akalazimika kutamka kuwa atafuta
ushuru unaoonekana kuwa kero.
“Nitafufua Chuo cha Kilimo Ukiriguru
na kutumia wataalamu wake
kuboresha kilimo cha pamba,”
alisema.
Mgombea ubunge Jimbo la Misungwi,
Charles Kitwanga alisema kuna sifa ya
Dk Magufuli ambayo haijatajwa nayo
ni ubunifu, kwani alianzisha mfuko wa
kujenga barabara kwa fedha za ndani
hali iliyowashangaza wafadhili.
“Hizi barabara tunazotaja kama siyo
yeye zisingekuwapo, mnakumbuka
wafadhili walikuwa wanakataa
kutukopesha, akaanzisha mfuko wa
kujenga barabara mpaka wafadhili
wanauliza fedha zitakapopatikana,
akawaambia tunazo,” alisema.
Kitwanga alimwomba mgombea huyo
kuwajengea hospitali ya wilaya na
kiwanda cha kusindika nyanya, zao
linalolimwa kwa wingi.
Akiwa Magu, Dk Magufuli alisema
endapo atachaguliwa, ataubadilisha
mji huo kwa kutatua kero sugu ya maji
na kujenga barabara zinazozunguka
mji huo. Alisema atatumia uwezo wake
wote kuhakikisha kilimo cha pamba
kinakuwa bora ili bei ya zao hilo
ipande na kuwanufaisha wakulima.
Akihutubia umati wa watu kwenye
Viwanja vya Sabasaba jana, Dk
Magufuli alisema: “Natambua kwamba
Magu shida yenu kubwa ni maji,
mmekuwa mkitaabika kwa muda
mrefu, huku Ziwa Victoria likiwa
limewazunguka.
“Kwa kutambua kwamba maji ni
muhimu kwa binadamu, hapa Magu
lazima mpate maji na tayari Kampuni
ya Cowi inafanya upembuzi yakinifu
kuhakikisha maji yanafika,
wakikamilisha tu suala la maji kufika
Magu niacheni mimi...”
Dk Magufuli alisema anataka kuona
Magu inabadilika na kwamba
ameahidi kujenga barabara
zinazozunguka mji huo na kuunganisha
wilaya jirani.
Alisema amezaliwa na kulima pamba
pamoja na kufuga, hivyo ni mtoto wa
mkulima na mfugaji na kwamba
atatumia uzoefu wake kuhakikisha bei
ya pamba inakuwa juu. “Nafahamu
kwamba bei ya pamba kwa sasa
imeshuka, lakini mimi ni mtoto wa
mkulima na mfugaji, pamba
naifahamu vizuri, nataka tutengeneze
mazingira mazuri kwa wakulima wa
pamba ili iwe bora,” alisema Dk
Magufuli.
Aliwataka wakazi wa mji huo, kula
fedha za watu wanaowahonga ili
wawachague, akisema hizo ni fedha
zao ambazo walizichuma kwa kutumia
ufisadi.
“Nyie mkipewa fedha kuleni, kwani
kula ni kwa mafisadi kulala kwa
Magufuli,” alisema na kuongeza kuwa
akichaguliwa, atakuwa rais wa watu
wote, kwa kuwa maendeleo hayana
chama.
Aliahidi kufuta ushuru ambao
umekuwa ukiwasumbua
wafanyabiashara ndogondogo
sambamba na kupunguza kodi za vifaa
vya ujenzi ili bei ya vifaa hivyo
ipungue na kuwawezesha wananchi
kununua na kujenga nyumba bora.
Imeandikwa na Aidan Mhando, Midraji
Ibrahim na Twalad Salum