Mshambuliaji wa Mbeya City, Haruna
Moshi ‘Boban’
Mbeya. Wakati Simba ikiibuka na
ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mbeya
City, imebainika kuwa Wekundu hao
wa Msimbazi waliingia uwanjani
wakiwaza namna ya kumkaba kiungo
wao wa zamani Haruna Moshi ‘Boban’.
Simba waliingia mchezo wakiwaza
Boban angeingia na jipya gani,
baadaye waligundua kiungo huyo
hawatishi kwani ameongeza uzito kiasi
cha kushindwa kuendana na kasi ya
mechi huo uliochezwa Uwanja wa
Sokoine.
Hiyo ilikuwa mechi yake ya kwanza
kwa Boban ya Ligi Kuu Bara msimu
huu baada ya kuchelewa kujiunga na
kikosi hicho na alifanya mazoezi siku
moja kabla ya mechi hiyo na kocha wa
City, Meja Mstaafu Abdul Mingange
kuamua kumtumia.
Wachezaji waliowahi kucheza naye
Boban akiwa Simba, akiwamo kocha
msaidizi, Seleman Matola na nahodha
wa timu hiyo, Musa Hassan ‘Mgosi’
walimwelezea Boban kuwa ni mchezaji
mzuri, ila kwa sasa anahitaji kuongeza
juhudi katika mazoezi kwani
anaonekana kuwa mzito kutokana na
mwili wake kuongezeka uzito.
“Boban nimemwona, ni mchezaji
mzuri, kikubwa anachopaswa
kukifanya kwasasa ni kuongeza
mazoezi, maana amekuwa na mwili
mnene, ila kiuwezo bado anaonekana
yupo fiti na anaweza kukubadilishia
matokeo muda wowote,” alisema
Matola.
Naye Mgosi alisema, “namfahamu
Boban, si mchezaji wa kubezwa
unapocheza naye, anaweza kukuliza
muda wowote, ila kwa sasa bado
hajapata mchezaji ndani ya Mbeya
City ambaye anaweza kumwelewa kwa
haraka uchezaji wa Boban ama nini
anataka anapokuwa uwanjani.
“Boban siyo mchezaji wa
kukimbiakimbia, jinsi anavyocheza
ndivyo hivyo hivyo, anavyoweza
kukufunga bila kutarajia, ila
namshauri aongeze mazoezi apunguze
mwili na atawasaidia Mbeya City kama
watamtumia vizuri,” alisema Mgosi.
Kocha mkuu wa Simba, Dylan Kerr
naye alisema kuwa amepata taarifa za
Boban kuwa ni mchezaji hatari na
anapaswa kuchungwa katika mechi
hiyo japokuwa hajawahi kumuona
akicheza.
“Tunashukuru tumeshinda mechi hii
na kupata pointi tatu, Mbeya City siyo
timu mbaya na wamecheza kwa
kiwango cha juu, ila hawajapata bahati
ya kutufunga.”
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni