Mgombea urais wa Chadema, Edward
Lowassa akihutubia mkutano wa kampeni
uliofanyika kwenye Uwanja wa
Rwandanzovwe, Nzovwe mjini Mbeya
jana. Picha na Emmanuel Herman
Mbeya/Mbarali. Mgombea urais wa
Chadema, Edward Lowassa amesema
amejiandaa na yupo tayari
kuwaongoza Watanzania akiwa rais wa
awamu ya tano.
Akizungumza kwenye Uwanja wa
Ruanda Nzovwe- Mbeya Mjini, Lowassa
alisema: “Ninatosha, nitumeni kwa
kura zenu… nipeni kura za kutosha
niwatumikie.”
Lowassa ambaye alisema anasikia deko
kutokana na wingi wa watu, alisema
misamaha ya kodi kwa sasa ni Sh1.6
trilioni na kwamba atahitaji Sh1.3
trilioni kati ya hizo kwa ajili ya elimu
itakayolipiwa na serikali kuanzia
chekechea hadi chuo kikuu.
Alirejea kusema kuwa katika serikali
yake hakutakuwa na michango ya
elimu, maabara wala madawati.
Akizungumza kabla ya kumkaribisha
Lowassa, Mwenyekiti wa Chadema,
Freeman Mbowe alisema viongozi
waliokuwa CCM akiwamo Lowassa,
wamejiunga na chama chao kwa kuwa
kina misingi imara.
Akizungumzia suala la upigaji kura,
alisema siku sita zilizobaki ni muhimu
kwa Watanzania kufanya uamuzi na
kusisitiza kuwa kuna kila sababu ya
kubakia kwenye vituo vya kura baada
ya kupiga kura huku akidai kwamba
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC),
haiko huru.
Sumaye
Akihutubia mkutano huo, Waziri Mkuu
mstaafu, Frederick Sumaye alimtaka
Waziri wa Uchukuzi, Harrison
Mwakyembe kuwasomea wananchi wa
Mbeya, ripoti ya Richmond kuona
kama Lowassa anahusika.
“Lowassa hahusiki, alijiuzulu kwa ajili
ya kuwakoa wao na wao wanaendelea
kuilipa Richmond kwa mgongo wa
Dowans wakati Lowassa hayupo,”
alisema.
Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph
Mbilinyi alisema tatizo kubwa kwa
wakazi wa jimbo lake ni maji hasa
katika vijiji vya Uyole na Mwakibete na
kusema kuna kila sababu ya kuvuta
maji kutoka Ziwa Nyasa hadi Mbeya ili
kukabiliana na tatizo hilo. Alisema
matatizo mengine ni hospitali na
huduma za afya akitaka wapatiwe
mashine za x-ray, CT Scan na umeme
wa uhakika.
Ilivyokuwa mchakamchaka
Kabla ya mkutano huo, Jiji la Mbeya
lilitawaliwa katika hekaheka za
mapokezi ya Lowassa kuanzia asubuhi
huku wakazi wakianza kufurika
kwenye uwanja huo tangu saa mbili
asubuhi.
Jiji lilitawaliwa na pilipika za
bodaboda na bajaji zenye bendera za
Chadema katika maeneo mengi
hususan Barabara Kuu ya Mbeya-
Zambia kuanzia Kabwe, Mwanjelwa,
Mafiati, Soweto na Mama John
ulikofanyikia mkutano huo.
Wafuasi wa mgombea huyo
walionekana wakirandaranda maeneo
mengi ya jiji hilo wakiwa wamevalia
sare za Chadema huku wakipiga deki
Barabara Kuu ya Mbeya - Zambia.
Muda mfupi kabla ya mkutano kuanza,
wafanyabiashara walifunga maduka
kwenda kusikiliza sera.
Wachuuzi wa vyakula na vinywaji
walihamishia biashara zao kwenye
mkutano huo tangu usiku wa kuamkia
jana na wengi walionekana kufurahia
uamuzi wao kutokana na biashara
waliyofanya.
Mmoja wa wauza chipsi, John Antony
alisema: “Aisee si unajua tena kufaa
kufaana, leo kuna neema kubwa kwetu
ndiyo maana leo tumehamishia
biashara yetu uwanjani.”
Mbarali
Katika mkutano wa Mbarali, wafuasi
wa CUF na Chadema walizua tafrani
wakati wakimsubiri Lowassa katika
Uwanja wa Mpira, Rujewa.
Tafrani hiyo ilizuka baada ya
mgombea wa CUF, Gamdust Haji
kufika na gari lake kisha kushuka na
wafuasi wanaomuunga mkono kwa
kumbeba juujuu na kumpeleka jukwaa
kuu, jambo ambalo liliwakera wafuasi
wanaomuunga mkono mgombea wa
Chadema, Liberatus Mwang’ombe na
kutaka kumuondoa kwa nguvu.
Polisi wazima rabsha
Baadhi ya mashuhuda walisema
kulikuwa na kundi la wafuasi
wanaomuunga mkono mgombea wa
CUF na kundi la mgombea wa
Chadema ambao walikuwa
wakilumbana huku kila upande
ukitaka mgombea wao ndiye anadiwe
na Lowassa kwa wananchi.
“Unajua hawa watu walishindwa
kuafikiana nani agombee ubunge
kupitia yale makubaliano yao Ukawa,
kitu ambacho kila chama kilisimamisha
mgombea wake,” alisema mmoja wa
wakazi wa Rujewa mjini, Athumani
Mwakitalima.
Akizungumzia suala hilo, Haji alisema:
“Ni kweli nimefanyiwa vurugu,
wamevunja vioo vya gari langu,
wakitaka niondoke kwenye mkutano
huo eti sina haki ya kushiriki na
kumsikiliza mgombea wangu wa urais.
Nimetoa taarifa polisi na kuna watu
wamekamatwa.”
Aliwalaumu viongozi wa kitaifa
walioambatana na Lowassa kwamba
hawakutaka kuuliza sababu za yeye
kutowapo mkutanoni hapo na badala
yake kumnadi Mwang’ombe akisema
hawakutenda haki.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni