Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Dk John Pombe Magufuli
Dar es Salaam. Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Dk John
Pombe Magufuli amefuta safari zote za
nje ya nchi kuanzia leo hadi hapo
maamuzi mengine yatakapotolewa.
Dk Magufuli ameagiza shughuli zote
zinazotakiwa kufanywa nje ya nchi
zifanywe na kusimamiwa na
mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania
nchi za nje.
Uamuzi huo wa rais ameutoa Ikulu
jijini Dar es Salaam katika kikao
kilichojumuisha watendaji
mbalimbali wa serikali wakiwemo
Makatibu wakuu, Manaibu Makatibu
wakuu, Gavana wa Benki Kuu na
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya
Mapato Tanzania (TRA).
Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu kwa
vyombo vya habari ruhusa ya safari
nje ya nchi inaweza kutolewa kwa
jambo la dharura ambalo hata hivyo
jambo hilo lazima lipate kibali cha
Katibu Mkuu Kiongozi.
“Badala yake rais ametaka ziara nyingi
zielekezwe kwenda vijijini ili
kuwawezesha watendaji kujua na
kutatua kero za wananchi” imesema
taarifa hiyo.
Katika kikao hicho, rais ameelekeza pia
mambo kadhaa ambayo watendaji hao
wanapaswa kuyasimamia, kuyawekea
mikakati na kuyapanga vizuri ili
yasimamiwe mara moja na Baraza la
Mawaziri atakaloliteua.
Mambo hayo ni pamoja na kuanza kwa
mikakati ya kuhakikisha wanafunzi
wote wanaanza kupatiwa elimu ya
bure kuanzia Januari mwakani.
Taarifa hiyo imetaja jambo la pili kuwa
ni suala la uratibu wa mikopo ya
wanafunzi wa elimu ya juu ambapo
ameagiza lifanyiwe kazi na mipango
yake ikamilike kwa ajili ya utekelezaji
mzuri zaidi.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, rais
amemuagiza Kamishna wa TRA
kusimamia kwa makini zoezi la
ukusanyaji wa mapato na kuhakikisha
kero ndogo ndogo zinazowakabili
wananchi zinaanza kushughulikiwa
mara moja.
Ameitaka TRA kukusanya mapato toka
kwa wafanya biashara wakubwa na
wakwepa kodi bila kuogopa mtu wala
taasisi yoyote na kusisitiza kuwa
hakuna mwenye mamlaka ya
kubatilisha maamuzi hayo zaidi yake.
Dk Magufuli ametaka usimamizi
mzuri katika suala la manunuzi ya
umma ambalo amesema limekuwa
likitumika vibaya na kuwa mwanya
wa maofisa wasio waaminifu kuiibia
serikali kwa kuongeza bei za bidhaa
na huduma tofauti na bei halisi ya
manunuzi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni