Mwenyekiti wa Chama cha Walimu nchini
(CWT) mkoani Manyara, Qambos Sulle.
Mirerani. Walimu mkoani Manyara
wametakiwa kujipanga ili wapate
huduma za fedha kwenye Benki ya
Walimu ambayo imepata leseni.
Benki hiyo inatarajiwa kuanza
kuwahudumia walimu na wananchi
wakati wowote kuanzia sasa.
Mwenyekiti wa Chama cha Walimu
nchini (CWT) mkoani Manyara,
Qambos Sulle aliyasema hayo wakati
akizungumza kwenye siku ya mwalimu
ambayo ilifanyika katika Mji Mdogo wa
Mirerani wilayani Simanjiro juzi.
Qambos alisema walimu ni wengi na
mishahara yao inapopitia kwenye
benki nyingine huwatengeneza faida
wamiliki wa benki hizo, hivyo
wanapaswa kutumia benki yao ili
iwanufaishe.
“Benki yetu pindi ikishaanza shughuli
zake tutazungumza na Serikali ili tuwe
tunapitisha mishahara ya walimu,
kwani watumishi tutakaowaajiri
tutawalipa kupitia makato ya benki,”
alisema.
Alisema huu ni wakati sahihi kwa
walimu kufaidi matunda ya jasho lao
kwa kuwa kupitia benki hiyo
watajiongezea kipato na kufanya
shughuli nyingine za maendeleo.
Akizungumza katika siku hiyo ya
mwalimu, Katibu wa CWT wilayani
Simanjiro, Abraham Kisimbi alisema
walimu wanapaswa kushughulikiwa
mahitaji yao ili waweze kutekeleza
majukumu ipasavyo.
Katibu wa CWT mkoani Manyara, Nuru
Shenkalwa alisema kwa sasa walimu
wengi ni vijana ambao wanajua haki
zao na wanasoma hadi mitandao,
tofauti na walimu walioanza kazi
miaka ya 1980 wanaotarajia kustaafu.
“Walimu wengi wa zamani walikuwa
wanategemea kusoma magazeti mawili
yaliyokuwapo, lakini hivi sasa kuna
hadi mitandao, hivyo walimu vijana
wanatambua namna ya kudai haki zao
za msingi,” alisema Shenkalwa.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni