Taifa lenye akiba ya kutosha na
uchumi imara linakuwa na uwezo
katika kujiletea maendeleo na hata
kustahimili majanga yoyote
yanapotokea. Nguvu hiyo inatokana na
uwezo mkubwa wa akiba na mtaji
iliyowekezwa kwenye miradi
mikubwa.
Mtu kuweka akiba, ni muhimu sana
kama vile ilivyo kwa taifa. Saikolojia ya
matumizi ya fedha inaonyesha kuwa
mtu hupenda kutumia sasa kuliko
kusubiri baadaye ambapo ingeongeza
faida na thamani zaidi.
Fedha ni kitu ambacho kipo tu kwa
muda kama mtu aliyekuwa nayo sasa
akishindwa kuidhibiti leo, kesho
hatakuwa nayo. Suala mtambuka hapa
ni je, kwa nini niweke akiba au
niwekeze kwa jambo lingine?
Ningependa nizungumzie juu ya njia
mbalimbali za kuweka akiba ambapo
zikitumika zinaweza kukuletea faida
kwa karne hii, japo kiuhalisia kwa
Waafrika kuweka fedha ni tatizo sugu
kwa walio wengi. Hali kama hii
inatokana na uwezo mdogo wa
kudhibiti fedha kwa mitindo ya kisasa
na kibiashara pia. Elimu juu ya jambo
hili haijafika au haijakaa vizuri katika
upande wa ubongo iliyo wazi kwa
mazingira ya hapa nchini.
Zipo njia ambazo ni nzuri zikitumika
kwa kuweka akiba kwa faida
zitaongeza maendeleo ya wengi. Njia
hizo ni:
Moja, ni kununua fedha za kigeni.
Mara nyingi fedha za kigeni mfano
Dola za Marekani, Euro, Pound ya
Uingereza na fedha kutoka Bara la Asia
kama vile za Saudi Arabia, huwa
zinapanda thamani ukilinganisha na za
Tanzania.
Mfano, ulinunua Dola moja ya
Marekani Novemba, mwaka jana kwa
Sh1,300. Mwaka huu unaiuza kwa
Sh2,100. Ukipiga hesabu umepata
faida ya Sh800. Kama ulinunua Dola
10,000, leo hii ikiziuza una faida ya
Sh1 milioni, na kadhalika.
Mtindo wa kununua dola kwanza
unapunguza kubeba lundo la fedha
nyingi, inakuzuia kuitumia bila
sababu, hivyo kuendelea kuwa akiba,
kukulinda na kukuwezesha uwe na
faida pale mfumuko wa bei
unapoongezeka na inaweza kukusaidia
iwapo itakulazimu usafiri nje ya nchi.
Ukisafiri nje ya nchi itakufanya
usitumie fedha nyingi za kununua za
kigeni kwa gharama kubwa.
Pili, ni simu benki. Huu ni mfumo
ambao upo sana siku hizi eneo la
Afrika Mashariki. Siku hizi kampuni za
simu zimewezesha mtu kuweka akiba.
Huduma imeboreshwa zaidi kwa
kuweza kuzihamishia kwenye akaunti
za benki, kulipia huduma na bidhaa au
kuzitoa katika nchi nyingine kulingana
na aina ya fedha za eneo husika.
Hii inamuwezesha hata kama mtu
akiwa mbali na benki na kuwa na
uwezo wa kuokoa muda kwa kutumia
pesa alizoweka kwenye simu yake kwa
kuzitoa kwa wakala aliye karibu naye.
Vilevile, kwa kutumia simu waweza
kuvuta fedha kutoka kwenye akaunti
yako ya benki na kuziingiza kwenye
simu yako na kuwa huru kuzitoa ili
kuzitumia eneo lolote kwa kutumia
mawakala.
Siku hizi pia kwa kutumia akiba
kwenye simu unaweza kupata huduma
nyingine kupitia simu hiyo kama vile
kununua umeme, kulipia bili ya maji,
matibabu, king’amuzi na hata tiketi za
kuingia kwenye michezo ya soka au
tamasha. Mtu aweza kudunduliza
fedha kidogokidogo kwenye simu yake.
Tatu, kuweka akiba kwa kutumia benki
na taasisi nyingine za kifedha. Hii
husaidia sana kuhamasisha huduma za
kuweka akiba kwa malengo kama vile
kumsomesha mtoto au amana.
Uwekaji wa fedha za namna hiyo pia
huweza kusaidia kuwa na fedha za
kukabili dharura na kuwa na mitaji
mikubwa ya kibiashara na hatimaye
kuleta maendeleo makubwa
yaliyokusudiwa.
Nne, ni kumkopesha mtu na kurudisha
kwa riba. Siku hizi aina hii ya
ukopeshaji imeenea sana, hasa mijini
na vyuoni. Hii imetokana na watu
kuzidi kukua sana kiuelewa,
wamebadili mwelekeo kutoka
kumkopesha mtu pasipo riba hadi
kuwa na faida.
Watu wameerevuka na kufahamu
kuwa fedha ya mwezi au wiki hii ni
tofauti na ya mwezi au wiki lijalo.
Tatizo lililopo ni kwamba hakuna
maandishi ya kukopeshana kwa walio
wengi kwa sababu za kujali utu. Lakini
ukweli ni kwamba wanadamu wengi
wana tabia ya kubadilika. Kama huna
maandishi ya kukopeshana itakuwa
vigumu kupata fedha zako pale
anapokuwa si mwaminifu.
Tano, ni kuwekea bima mali zako na
biashara yako. Hii ni njia ambayo ni
muhimu sana maana hakuna mtu
anayeweza kuzuia majanga ambayo ni
ya asili au ya kawaida, hivyo bima
hasaidia sana siku ukipata ajali ya
biashara kwa kuibiwa au kuungua.
Sita, ni kununua vitu kama nyumba,
ardhi na vifaa vya gharama vyenye
kudumu muda mrefu. Hivi waweza
kuviuza baadaye kwa bei ya juu.
Maendeleo ya mtu mmojammoja ni
mafanikio ya taifa. Taifa lenye akiba ya
kutosha kwa kawaida linakuwa imara
na wananchi wenye akiba kwa njia
mbalimbali kama nilivyoorodhesha, ni
watu wenye maisha ya uhakika.
Dharura zote wanaweza kuzikabili na
hapa ndipo pia mitaji mikubwa ya
biashara inatokea. Kuweka akiba ni
jambo la msingi, tuanze leo kuweka
akiba. MPENZI MSOMAJI KAMA UMEGUZWA NA MAKALA HAYA TUANDIKIE KWENDA EMAIL HII kimarioerasmi@gmail.com