Mbunge wa viti maalumu wa Chadema,
Rose Kamili akizungumza na waandishi wa
habari jijini Dar es Salaam jana kuhusu
kauli aliyoitoa aliyekuwa katibu mkuu wa
Chadema, Dk Willibrod Slaa . Kushoto ni
binti wa Dk Slaa, Emiliana Slaa na Linus
Slaa. Picha na Venance Nestory
Dar es Salaam. Kauli ya Katibu Mkuu
wa zamani wa Chadema Dk Willibrod
Slaa kuhusu hatma yake kisiasa
imeendelea kutikisa baada ya mke
wake wa zamani, Rose Kamili kuibuka
na kusema amesikitishwa na kauli
alizozitoa mume wake huyo
alipozungumza na waandishi wa
habari Septemba Mosi.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana,
Kamili alisema wakati Dk Slaa
anatangaza kung’atuka kwenye siasa
alisema amekuwa akila mihogo na
familia yake, jambo ambalo si la kweli.
Alisisitiza kuwa japokuwa mihogo siyo
chakula kibaya lakini watoto wake,
Elimiana na Linus Slaa hawakuwahi
kuishi kwa kutegemea chakula hicho
ingawa walitelekezwa na baba yao
tangu mwaka 2010.
Kamili ambaye pia ni mbunge wa
kuteuliwa wa Chadema, alisema Dk
Slaa aliwadanganya wananchi
aliposema kuwa haongei na mgombea
wa urais wa Chadema anayeungwa
mkono na Ukawa, Edward Lowassa na
Waziri Mkuu wa zamani Frederick
Sumaye kuwa siyo kweli kwa kuwa
amekuwa akiwasiliana na viongozi hao.
Alisimulia kuwa mwaka 1995 wakati
Dk Slaa alipoenguliwa na CCM
kugombea ubunge Jimbo la Karatu,
alikwenda nyumbani kwa Lowassa
kuomba ushauri.
“Lowassa alisema ‘mimi nakushauri
ujiunge na chama chochote’” alisema
Kamili na kuongeza kuwa marafiki
zake Dk Slaa nao walimshauri aingie
chama chochote.
“Mimi namshangaa anavyosema
haongei na Lowassa… hizo chuki
anazosema yeye kama padri mstaafu
zinatoka wapi?,” alisema Kamili.
Kuhusu Sumaye, Kamili alisema kuwa
wiki tatu zilizopita alipigiwa simu na
kiongozi huyo akimuulizia namba ya
Dk Slaa, baada ya kumtafuta kwenye
simu yake bila mafanikio.
“Aliniuliza mbona simu yake
haipatikani, nikampa akampigia
wakaongea,” alisema.
Mjini Bukoba, Askofu Msaidizi wa
Jimbo Katoliki la Bukoba, Methodius
Kilaini amesema anamshangaa Dk Slaa
kutoa tuhuma dhidi ya maaskofu kwa
kuwa aliwahi kuwa Katibu wa Baraza
la Maskofu na anajua wanavyofanya
kazi.
Akizungumza katika mahojiano
maalumu na Mwananchi mjini Bukoba,
Askofu Kilaini alisema Maaskofu
hawanunuliki na kanisa halifungamani
na upande wowote wa kisiasa huku
akidai huenda kauli hiyo ilimponyoka.
Kauli ya Askofu Kilaini imetolewa
ikiwa ni baada ya siku chache
zilizopita aliyekuwa Katibu Mkuu wa
Chadema, Slaa kutangaza kustaafu
siasa huku akiwatuhumu baadhi ya
maaskofu kupokea rushwa kutoka kwa
mmoja wa wagombea.
‘’Wanasiasa ni wachangiaji wazuri
katika hafla mbalimbali za kanisa
lakini hata siku moja huwezi kusema
maaskofu wamenunuliwa Kanisa
linashikilia maadili na kuombea amani
kwa Taifa,’’ alisema Kilaini
Pia Askofu Kilaini aliongeza kuwa
matamko kama yaliyotolewa na Dk
Slaa yanaweza kusababisha
mkanganyiko kwenye jamii, huku
akionya hatari ya dini kutumika
kwenye mijadala kuelekea Uchaguzi
Mkuu.
Aidha alirejea mwaka 2000 kuwa
baada ya vurugu kuanza kutokea
Zanzibar na wananchi kukimbia,
waliitana viongozi wa madhehebu yote
ya dini na kutoa tamko la pamoja
wakionya dini zisihusishwe kwenye
harakati za kisiasa.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni