other blog

Jumatatu, 14 Septemba 2015

Makala... story ya waziri ambaye alikuwa mchawi inaendelea hapa.. usikose nakala yako kwenye gazeti la ijumaa kila ijumaa kwa simulizi za kweli ... inaandaliwa na WASONGA MROMBO .. Mjinga wa rombo

ILIPOISHIA IJUMAA:
Waziri Meshack alishaniona , akatoka na
kuja kunilaki kwenye mlango wa gari.
“ Karibu mchungaji ,” akaniambia huku
akitabasamu.
Niliposhuka kwenye gari nilifuatana naye
hadi sebuleni mwake .
“ Karibu ukae ,” Meshack akaniambia .
Nilikaa katika kochi moja na yeye akakaa
kwenye lingine akinielekea mimi.
“ Nimeshukuru kuwa umeitikia wito
wangu, sijui nikupatie kinywaji gani ?”
Waziri Meshack akaniuliza .
“ Hapana. Sihitaji kinywaji chochote .
Asante sana. ”
SASA ENDELEA …
Waziri akanyamaza kimya kama vile
alikuwa akitafuta jinsi ya kuanza
kuniambia alichokuwa anataka kuniambia .
Zilipita kama sekunde nne au tano kisha
ghafla akasema .“ Mchungaji samahani
sana. Nilipaswa kukueleza niliyonayo
ofisini kwako lakini kwa vile wewe ni
mtumishi wa Mungu umekubali kuja
nyumbani kwangu kunisikiliza . Kwa hilo
nakushukuru sana. ”
Alinyamaza kidogo , akiendelea kufikiri
kisha akaendelea.
“ Binadamu ni binadamu si malaika ambao
hawatendi dhambi wala hawakosei.
Binadamu unaweza kumkosea Mungu na
hilo linawakuta watu wengi lakini Mungu
humpenda yule mkosefu anayejirudi,
akatubu dhambi zake. Na kutubu ni lazima
kuungama kama ambavyo mimi nataka
kufanya kwako wewe hii leo. ”
“ Umesema maneno ya Kimungu .
Nakubaliana na wewe kwa asilimia mia
moja kwamba kutenda dhambi ni
majaribu ya shetani . Lakini roho mtakatifu
anaweza kukuongoza ukafikia mahali
ukasema sasa narejea kwa Mola wangu.”
“ Ni kweli mchungaji . Sasa ninataka
kuungama makosa yangu na pia ninahitaji
maombi ili ile hatari ambayo ninaiona iko
mbele yangu isinisogelee tena .”
“ Sawa. ”
“ Kwanza nitaanza kukuelezea historia
yangu. Nimefahamika kwa Watanzania
baada ya kuwa waziri lakini maisha yangu
ya nyuma hayatambuliki. “ Mimi ni mzaliwa
wa Kijiji cha Mbogwe Wilaya ya Nzega
mkoani Tabora . Baba yangu Mzee
Shangwe (si jina lake halisi) alifariki dunia
nikiwa darasa la saba. Nikalelewa na babu
yangu Mzee Ngasa ( pia si jina lake halisi) .
Mzee Ngasa aliendelea kunisimamia
masomo yangu hadi nikaingia chuo kikuu .
Lakini wakati namaliza kidato cha sita,
babu yangu aliniita na kuniambia jambo
ambalo lilinishitua .
Ilikuwa usiku. Aliniita chumbani kwake ,
akaniambia .
“ Nataka kukueleza jambo zuri mjukuu
wangu. Naona sasa umekua mkubwa,
unapaswa kujua mambo ambayo yatakuja
kukuhusu sana .”
Aliponiambia hivyo , kidogo nilishituka.
Nikamuuliza.
“ Ni jambo gani hilo babu?”
“ Mjukuu wangu umezaliwa katika familia
ya wachawi,” akaniambia .
“ Nimezaliwa katika familia ya wachawi?”
“ Ndiyo .”
“ Ni nani na nani ni wachawi katika familia
yetu?”
“ Baba yako alikuwa mchawi na uchawi huo
nilimfundisha mimi babu yako. ”
Maneno ya Mzee Ngasa yalinikumbusha
mambo kadhaa ambayo nilikuwa nikiyaona
pale nyumbani siku za nyuma . Nilipokuwa
ninaingia chumbani mwa babu wakati
mwingine hukuta vitu visivyo vya
kawaida.
Kuna siku nilikuwa natafuta panga,
nikachungulia uvunguni mwa kitanda cha
babu nikashituka kukuta mkono wa mtoto
mchanga uliokaushwa na kuwa kama
kijiko. Pia nilikuta ngozi ya kichwa cha
binadamu ikiwa na nywele zake.
Kitu kingine nilichokiona hakikuwa cha
kawaida kwa babu, alikuwa akienda kulima
shambani kwake usiku . Hupenda
kuondoka nyumbani usiku wa manane na
kurudi wakati wa alfajiri. Nilipokuwa
namuuliza babu unakwenda wapi ananijibu
kuwa anakwenda shamba .
Hivi vitu vilianza kunitia shaka mapema
sana kuwa babu yangu hakuwa mtu wa
kawaida. Hivyo siku ile aliponiambia kuwa
yeye ni mchawi lilikuwa jambo ambalo
nilianza kulishuku tangu siku za nyuma .
Babu akaendelea kuniambia .
“ Nilidhani ningekufa kabla ya baba yako .
Nilikuwa nimemuandaa yeye kurithi
mfuko wangu wa uchawi lakini akatangulia
kufa yeye kabla yangu.”
Babu akanyamaza kidogo na kunitazama
usoni kwangu . Alipoona sikuwa
nimeshituka sana akaendelea kuniambia .
“ Baba yako nilimfundisha uchawi lakini
hakuwahi kutoa kitu . Sasa mimi nilitakiwa
nikutoe wewe nikakataa.”
“ Sijakuelewa babu. Umeniambia baba
yangu hakuwahi kutoa kitu na wewe
umetakiwa unitoe mimi. Hebu fafanua
hapo babu.”
“ Yeye aliwahi kula nyama za wenzake .
Ukiwa mchawi ni lazima umtoe kafara
mwanao au mtu wako wa karibu ili
mumle. Yeye hakuwahi kutoa kafara mtu
yeyote. Badala yake nikaambiwa mimi
nikutoe wewe…”
“ Yaani babu unitoe mimi niliwe na
wachawi?” nikamuuliza babu kwa
mshituko .
“ Lakini nimekataa. ”
“ Hata mimi nisingekubali upumbavu huo . ”
“ Pale unapotakiwa unakuwa huna ujanja
mjukuu wangu. Utaonekana umekufa .
Ukienda kuzikwa, usiku tunakwenda
kufukua kaburi tunakuchukua. ”
“ Kwa hiyo mnakula nyama za maiti?”
“ Mbona ni kawaida mjukuu wangu. Kwani
utajua kama ni nyama ya maiti? Ni nzuri
sana.”
“ Sasa ulipokataa kunitoa wakakuambia
nini?”
“ Kwanza unapotakiwa kutoa mtu wako
huwezi kukataa ila mimi nilitoa hoja
zangu . Nilisema kwamba wewe
nimeshakuandaa kuwa mrithi wangu na
katika familia yetu umebaki wewe peke
yako. Nikawaambia kwamba karibuni
utaoa mke na mtoto utakayezaa kwanza
ndiye tutamtoa . Hapo ndiyo
walinikubalia.”
Maneno ya babu yalinikumbusha ule
mkono wa mtoto mchanga nilioukuta chini
ya mvungu wa kitanda chake na ile ngozi
ya kichwa iliyokuwa na nywele. Kutokana
na maelezo yake niliamini kwamba ule
mkono ulikuwa wa maiti ya mtoto
iliyofukuliwa na ile ngozi yenye nywele
ilichunwa kutoka katika kichwa cha
marehemu ambaye pia alikuwa
ameshazikwa .
“ Sasa ili kuyasitiri maisha yako na ili
nionekane mkweli nataka nianze
kukufundisha hii kazi ili wewe uwe kama
mimi,” babu akaniambia .
Baada ya kuyatafakari maneno yake kwa
makini nilimwambia .
“ Sikiliza babu…”
Je, nini kitaendelea? Usikose Ijumaa
kwenye Gazeti la Ijumaa .
Je, nini kiliendelea ? Usikose kufuatilia
Ijumaa kwenye Gazeti la Ijumaa .


USIKOSE KUTEMBELEA PAGE HII IJUMAA ILI KUPATA MWENDELEZO WA SIMULIZI HIYO.... ROMBO MPOOOO.....LIKE PAGE YETU YA FACEBOOK ... www.facebook.com/eaglefm97 uunganishwe na mamia ya warombo kwa maendeleo ya wilaya yetu ya rombo ... na kukomesha tabia ya kusengenywa kwamba tumeshindwa kazi ... tupia like yako sasa...

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni