Kamanda wa Polisi Pwani, Jafar Mohamed
Kibaha. Mamia ya abiria waliokua
wanasafiri kupitia barabara kuu ya
Dar esalam - Morogoro leo
wamekwama kwa zaidi saa nne katika
eneo la Bamba Kata ya Kongowe mjini
Kibaha baada ya magari matano
kugongana na kisha kuziba barabara.
Katika ajali hiyo abiria watano
wamejeruhiwa sehemu mbalimbali za
mwili huku wanne kati yao wakiwa
wamevunjika mikono na miguu
ambapo majeruhi wote wamepelekwa
katika hospitali teule ya rufaa ya
Tumbi kwa matibabu.
Kamanda wa Polisi Pwani, Jafar
Mohamed amethibitisha kutokea kwa
tukio hilo na kusema ilitokea majira
ya saa 10.50 alfajiri ya leo na kwamba
barabara ilifunga kutokana na moja ya
magari yaliyogongana kuziba
barabara.
Kamanda Jafar alifafanua kuwa hatua
hiyo ilisababisha mabasi,malori na
magari mengine madogo kushindwa
kuendelea na safari kwa wakati katika
barabara hiyo.
"Ni kweli kuna usumbufu uliotokea
kwa wasafiri wa mikoani hasa wale
waliosafiri na magari yaliyotoka
alfajiri kwenda mikoani katika
barabara hii,” alisema kamanda huyo.
Kamanda huyo amewataja majeruhi
hao kuwa ni Abdul Mashaka
aliyevunjika mkono wa kulia,Juma
Hajji aliyevunjika mguu wa kulia,
Halfani Abdalla aliyevunjika miguu,
Zakaria Ramadhani na Othuman
Omary na wote walipelekwa kutibiwa
hospitali yaTumbi.
Awali Mkuu wa kikosi cha usalama
barabarani mkoani Pwani, Isango Abdi
alisema magariyaliyohusika na ajali
hiyo ni aina ya Fuso, Scania tanker na
Iveco tanker.
Alibainisha kuwa askari walifanikiwa
kudhibiti wizi wa mafuta katika malori
hayo na hivyo uharibu uliotokea ni
majeruhi na magari kuharibika.
Aliongeza kuwa chanzo cha ajali hiyo
ni dereva wa mojawapo ya lori
Raymond Mtega kuyapita gari zaidi ya
moja bila tahadhari na kufafanua
kuwa dereva huyo ameshakamatwa na
anahojiwa na baadae hatua za kisheria
zitafuata dhidi yake,
Naye Mwenyekiti wa Mtaa wa Bamba
ilipotokea ajali hiyo Amri Mavalla
alisema serikali ya mtaa kwa
kushirikiana na polisi walifanikiwa
kuyaondoa malori hayo yaliyoziba
barabara na saa 2.30 asubuhi magari
yote yaliyokuwa yamekwama eneo hilo
yaliendelea na safari kama kawaida.
-
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni