other blog

Jumatatu, 21 Septemba 2015

Fahamu kuhusu historia ya wachaga,chanzo na asili yao pekee kupitia eaglefm na mwandishi wetu malya ..mwandishi wa kitabu cha historia marangu.imeeandaliwa na wasonga mrombo




Kabila la Wachaga linafahamika kwa
wengi kuwa linapatikana mkoani
Kilimanjaro.Kwa asili, Wachaga ni
mchanganyiko wa Wamasai,
Wasambaa, Wataita, Wakamba na
Wakahe.
Wachaga walianza kuhamia kwenye
miteremko ya Mlima Kilimanjaro
kwenye karne ya 17.
Walipofika wakiwa katika vikundi
vidogovidogo waliwakuta wakazi,
wenyeji kwenye Misitu ya Mlima
Kilimanjaro walioitwa ìWakonyingo..
Wenyeji hawa ambao huitwa
Mbilikimo hawakupenda
kuchanganyika na wahamiaji wageni,
hivyo wakahama na kuanzisha makao
yao ya kudumu kwenye misitu
minene iliyopo nchini Kongo.
Watu wengi wanafikiria kwamba
Wachaga wanatokana na asili moja.
Ukweli ni kwamba wamegawanyika
katika himaya 15, wanatofautiana
kwa lafudhi, lugha, rangi na
mwonekano wa miili yao.Wachaga
wapo katika makundi makuu matatu
ya Hai, Vunjo na Rombo.
Wale wanaopatikana eneo la Hai ni
Wasiha, Wamasama,
Wamachame,Wangíuni, Wakibosho,
Wauru na Wamoshi. Kwa wale
wanaopatikana eneo la Vunjo ni
Wakirua, Wakilema, Wamarangu,
Wamamba na Wamwika.
Kutoka eneo la Rombo ni Wamkuu,
Wamashati na Wasseri.
Hadi sasa haijulikani vizuri asili ya
jina Wachaga, ila wanahistoria
wanaeleza kwamba jina hilo
linatokana na neno la Kiswahili
linaloitwa 'Kichaka'.
Inaelezwa kwamba misafara ya
wafanyabiashara iliyokuwa
ikiongozwa na Waswahili pamoja na
Waarabu, walipokuwa wakipita
maeneo ya Vunjo waliwaona wenyeji
wa huko wakiwa wamejenga vibanda
vya kulinda mazao yao yasiliwe na
wanyama waharibifu.
Wakawaita wenyeji hawa kwamba
wanaishi vichakani na kuanzia hapo
wageni wafanyabiashara na
Wamisionari walipokuwa wanakuja
Kilimanjaro walielekezwa na
waongozaji misafara yao kwamba
wanakwenda kwenye nchi ya
ìUchakani,î, wakimaanisha kwamba
kwa watu wanaoishi vichakani.
Hatimaye wageni wakashindwa
kulitamka vizuri neno hili na kuliita
ìUchagani,
Jina hili likawekwa kwenye ramani
na kuitwa nchi ya ìWachaga.î Hivyo
ndivyo wenyeji waliokuwa wakiishi
kwenye Miteremko ya Mlima
Kilimanjaro walivyopewa jina lao.
Wachaga.
Maendeleo ya Wachaga
Maendeleo yao hapo awali yalitokana
na zao la kahawa. Walifanikiwa
kuanzisha vyama vya ushirika na
hatimaye mwaka 1932 walianzisha
Halmashauri ya Wachaga (Chaga
Council) ambayo kwa sasa inatumiwa
na Halmashauri ya Wilaya ya Moshi.
Halmashauri hii iliongozwa na Mangi
Mkuu ìMshumbue Thomas Marealle
II.
Mwaka 1946, utawala wa Waingereza
uliboresha Baraza la Halmashauri ya
Wachaga. Himaya ndogo za Wachaga
zipatazo 17 (himaya mbili za
Wakahe na Waarusha chini
zilijumuishwa kwenye Tarafa ya
Vunjo) na kuundwa kwa Tarafa tatu
za Hai, Vunjo na Rombo.
Halmashauri ya Wachaga ilijenga
miundombinu na huduma za jamii
ikiwamo kuwasomesha watoto wao
kwenye shule na vyuo mbalimbali
kama Chuo Kikuu cha Makerere,
Uganda.
Halmashauri ya Uchaga ilikuwa na
bendera yake ambayo ipo hadi leo
kwenye Halmashauri ya Wilaya ya
Moshi, yenye nembo tano kuu:
1- Mlima Kilimanjaro uliochorwa
katikati ya bendera ukionyesha
mandhari nzuri ya kilele cha Kibo.
Kilele cha Kibo kinatoa maji safi na ni
kielelezo cha umoja wao.
2- Chini ya kilele cha Kibo, upande
wa kushoto wa bendera kuna
mgomba wenye ndizi. Hiki ni chakula
kikuu cha Wachaga.
3- Upande wa kulia wa bendera ni
tawi la mbuni ukiwa na matunda
yake. Kahawa ni zao lililowaletea
maendeleo.
4- Bendera imezungukwa na
matawi ya 'sale' lenye matawi mawili
(draceana plant). Matawi haya
yamefanya mduara kuzunguka kilele
cha Kibo, mgomba wa ndizi na tawi la
zao la kahawa. Masale ni mmea
unaoheshimiwa sana na Wachaga
wote.
Ni alama ya amani. Masale hutumika
katika sherehe na shughuli zote za
kimila zinazofanywa na Wachaga.
Majani yake ni kijani kibichi
yanayoonyesha jinsi Kilimanjaro
ilivyo na rutuba nzuri inayostawisha
mazao ya kila aina.
5- Juu kidogo ya kilele cha Kibo
yupo chui ambaye amejipumzisha.
Chui ni alama kuu ya mamlaka ya
Wachaga.
Hapo awali kwenye miteremko ya
Mlima Kilimanjaro walikuwepo chui
wengi wa rangi nyeusi lakini
kutokana na ongezeko la watu
pamoja na uharibifu wa mazingira
chui hawa wametoweka.
Sikukuu ya Wachaga
Sikukuu ya Wachaga wote ilikuwa
ikiadhimishwa Novemba 10 kila
mwaka kama kumbukumbu ya siku
ambayo Wachaga wote
walipokusanyika na kumchagua
Mangi Mkuu baada ya kuteuliwa na
Halmashauri Kuu ya Uchaga.
Maadhimisho ya kwanza ya mwaka
1952 yalitanguliwa na uchaguzi wa
Halmashauri ya Wachaga wote
kuanzia kwenye ngazi ya Uchili
(kijiji), Umangi ( uchifu wa eneo) na
mwisho ngazi ya baraza kuu.
Sherehe ziliadhimishwa mjini Moshi
ambako Wachaga wote pamoja na
wageni waalikwa kutoka mataifa
mbalimbali walikusanyika katika
Viwanja vya Halmashauri ya Uchaga
(sasa ni makao makuu ya
Halmashauri ya Wilaya ya Moshi,
[Kilimanjaro District Council-KDC])
kushuhudia sherehe kubwa na yenye
kusisimua sana.
Jumba la Makumbusho
Upo umuhimu mkubwa wa kuhifadhi
historia ya Wachaga kama
kumbukumbu sahihi kwa vizazi vya
sasa na vijavyo.
Pia, ipo haja kwa majengo ya
Halmashauri ya Wilaya ya Moshi
pamoja na Ikulu yakarejeshwa kwa
Wachaga ili yageuzwe kuwa majengo
ya kuhifadhi kumbukumbu ya kabila
hilo.
Katika majengo haya patahifadhiwa
nyaraka zote za Chaga Council
ambazo baadhi zimeshaanza
kutoweka, kutahifadhiwa pia
shughuli za mila na kiutamaduni
tangu enzi ya karne ya 18.
Halmashauri ya Wilaya ya Moshi
haina budi kutafuta eneo la kujenga
majengo mapya badala ya kuyatumia
ya kihistoria.
*Mallya ni mchambuzi wa masuala
ya maendeleo ya jamii na
mwandishi wa kitabu cha
Wamarangu na Maendeleo. -0754
390 402, email:
exaudmalya@yahoo.co.uk au kimarioerasmi@gmail.com

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni