Watoto wakicheza katika jalala eneo la
Bugando Mwanza, mazingira ya namna hii
ni hatari kwa afya zao.
Dar es Salaam. Idadi ya watu
waliopoteza maisha kwa ugonjwa wa
kipindupindu imeongezeka na kufikia
17 baada ya watu wengine wawili
kupoteza maisha jana.
Hata hivyo, idadi ya watu
walioripotiwa kuugua ugonjwa huo
tangu ulipuke katika Jiji la Dar es
Salaam Agosti 17, imefikia 2,000.
Ofisa Habari wa Manispaa ya Temeke,
Joyce Msumba alisema kuwa jana
walipokea wagonjwa wapya saba na
kati yao, mmoja ameshafariki dunia.
Msumba alisema wagonjwa wengi
hawatoki katika Manispaa hiyo bali
wapo wanaotoka eneo la Buguruni
katika Manispaa ya Ilala na
Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga
mkoani Pwani.
Alisema tayari wameshatoa taarifa
kwa maofisa wa afya wa wilaya zao ili
wafuatilie hali katika familia zao.
Mganga Mkuu wa Manispaa ya
Kinondoni, Victorina Ludovick alisema
wamepokea wagonjwa wapya 31 idadi
inayofanya watu waliolazwa katika
kambi ya ugonjwa huo kufikia 38.
Dk Ludovick alisema wagonjwa wengi
wanatoka maeneo ya Buguruni,
Vingunguti, Jangwani, Ilala,
Mchikichini, Tabata na Kigogo.
Alisema kuendelea kusambaa kwa
ugonjwa huo kunatokana na wakazi
wengi wa maeneo hayo kutozingatia
kanuni za afya wanazofundishwa na
wataalamu.
“Magari ya matangazo yanapita katika
mitaa yao kila siku kutoa elimu na
kuwahamasisha kunawa mikono kwa
sabuni baada ya kutoka chooni,
kuchemsha maji ya kunywa na
kuzingatia usafi wanapoandaa
vyakula,” alisema Ludovick
Alisema maofisa afya wanaendelea na
kazi ya kukagua mazingira
wanayofanyia kazi wafanyabiashara
wa vyakula na matunda ili kuwabaini
wanaokiuka agizo la kuacha kufanya
biashara hiyo hadi ugonjwa huo
utakapokwisha.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni