other blog

Jumamosi, 7 Novemba 2015

Prof Jay: Vijana ndiyo

Mbunge mteule wa Jimbo la Mikumi,
Joseph Haule, maarufu Profesa Jay
Mbunge mteule wa Jimbo la Mikumi,
Joseph Haule, maarufu Profesa Jay
amesema vijana ndiyo watakaoleta
mabadiliko nchini.
Akizungumza mwanzoni mwa wiki hii,
Profesa Jay, ambaye ni mbunge mteule
wa Jimbo la Mikumi kwa tiketi ya
Chadema, alisema vijana wanatakiwa
kujituma ili kuwa chachu ya
mabadiliko katika taifa lao.
Alisema jambo hilo wanatakiwa
kulifanya sasa bila kujali itikadi za
vyama vyao.
Profesa Jay, ambaye alipata umaarufu
kutokana na kibao chake cha kisiasa
cha “Ndio Mzee”, alisema kukaa
vijiweni na kulalamika hakuwezi kuwa
suluhu ya matatizo yao, hivyo
wakijituma kufanya kazi kwa pamoja
watawezesha Taifa kusonga mbele.
Profesa Jay alisema kuwa na malengo
ni njia mojawapo itakayomwezesha
kijana kujitambua na kujituma katika
kile anachokifanya, ili kutimiza
malengo aliyojiwekea kwa kipindi
mwafaka.
“Ukiangalia vijana maeneo ya vijijini
wanakuwa na malengo ya kuhakikishe
wanafanya mambo kadhaa kama
‘kujenga nyumba yangu ya kuishi
ndipo nioe mke’. Hii ni tofauti na
vijana wengi wa mijini. Naamini hata
wao wakiweka malengo Taifa litasogea
mbele kutoka hapa tulipo,” alisema
Profesa Jay.
Alieleza kuwa kijana yeyote anayeona
ana uwezo wa kufanya mabadiliko
anatakiwa kufahamu kuwa siasa
imeisha na huu ni wakati wa kufanya
kazi.
Alisema kwa sasa mabadiliko ni lazima
ili kuyavuta maendeleo kwani ndiyo
kitu cha msingi zaidi, akibainisha
kwamba ni kwa vijana wote nchini na
si Mikumi pekee.
“Mimi ni kijana nimefikiria kufanya
kazi itakayowakwamua vijana wote
nchini, nathamini uamuzi na namna
walivyoniamini wananchi wa Mikumi
kwa kunipa nafasi niwaongoze, lakini
natambua uwapo wa vijana Tanzania
nzima,” alisema Profesa Jay.
Alisema anachoweza kufanya sasa ni
kuwasaidia wasanii wenzake
kuwasemea na kutafuta njia za
kuwakomboa.
Hata hivyo alisema licha ya kuingia
katika siasa hana mpango wa
kuachana na muziki.
“Wapo wachungaji ambao waliingia
katika siasa hawakuacha kuhubiri,
wapo wafanyabiashara ambao nao
waliingia huko hata nao hawakuacha
biashara zao, kwa upande wangu
siwezi kuacha nitaendelea kufanya
muziki mpaka mwisho wa maisha
yangu,” alisema Profesa Jay.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni