other blog

Jumamosi, 7 Novemba 2015

Ikulu kutamu kwa

Kuna sura inayokinzana katika eneo la
Afrika Mashariki na lile la Kati. Kuna
wakati wanasiasa wanabisha kwenye
eneo hilo. Pia, bado kuna mwangwi
unaosukuma juu ya kile kinachoitwa
‘mabadiliko ya nyakati’.
Wote wanaozunguka eneo hilo
wanavuta subira kujua hatma yake.
Hata hivyo, kwa Rais Paul Kagame wa
Rwanda ni kama vile tayari
amechochea gia. Anajiandaa kukoleza
moto gari lake ili asonge mbele zaidi.
Inawezekana wakati huu anawatupia
macho wenzake. Anaendelea
kuwakodolea tena anawasimanga
moyoni. Lakini bila shaka anaamini iko
siku watafaulu na hatimaye kufuata
mkondo wa kisiasa zake.
Wenzake wanaendelea kupingana
kuanzia kwenye vikao vya Bunge hadi
majukwaa ya wazi ya kisiasa.
Pia, wanaendelea kutumia mifumo
‘dhaifu’ ya kisheria kuendelea
kupenyeza ushawishi wao. Wana kiu
kubwa tena wanaendelea kuwajaza
hamasa wananchi ili waendelea
kusalia madarakani.
Mengi yanaendelea kujitokeza barani
Afrika. Mathalani, Rais Joseph Kabila
wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo
(DRC), bado haamini kama atafaulu.
Jaribio lake la awali kulishawishi
Bunge kubadilisha Katiba ili awanie
muhula mwingine wa tatu wa uongozi
lilizua mzozo mkubwa na hata
kusababisha ‘vurumai na kujitokeza
harufu ya kutoweka kwa amani’.
Jaribio hilo sasa ameliweka kando
huku akiendelea kupima kina cha maji
kwa kijiti.
Wale wanaomjua wanasema kuwa Rais
Kabila anachanga upya karata zake.
Wanasema huenda akaibuka
‘kivingine’.
Wanasisitiza kuwa Rais Kabila bado
hajakata tamaa tena anasukumwa na
kile kilichojitokeza kwa Rais Kagame.
Rais Kagame ameidhinishwa na Bunge
kuendelea kuwania madaraka kwa
muhula mwingine wa miaka saba.
Pia, kuna wale wanaamini kuwa, Rais
Kabika inawezekana yupo kwenye
tafakuli kubwa.
Wanaamini kuwa huenda kiongozi
huyo akabadilisha mchezo na
kuwashinda wapinzani wake kwa
kutumia ‘mkakati mgumu’ uliotumiwa
na Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi.
Licha ya kuwa mazingira ya kisiasa
kwa nchi hizo mbili yanabeba sura
mbili zinazotofautiana lakini siasa
hupenda kuazima matukio. Siasa ni
harakati ya kuhodhi madaraka. Daima
siasa ni mchezo wa kuwinda dola.
Inavyoonekana Rais Kabila shauku
yake kubwa ni kufuata mkondo wa
jirani yake Rais Kagame.
Rais Kagame amefunguliwa mlango
kuendelea kusalia madarakani. Bunge
limeidhinisha marekebisho ya Katiba
na hivyo kumpa fungua wa kuendelea
kukalia kiti cha ‘enzi’ kwa utawala wa
Rwanda.
Wenyewe Rwanda wanamsifu
wakisema ni kiongozi aliyebeba
‘mkono wa chuma’.
Rais Pierre Nkurunziza amejitwalia
funguo. Amewapiga chenga wapinzani
wake na kuendelea kushikilia ufunguo
wa kusalia madarakani. Licha ya
kuandamwa na shinikizo kutoka
nyumbani hadi katika duru za
kimataifa, Rais Nkurunziza hakusita
kuendelea na mkakati wake. Aliusuka
mpango na kisha kuutekeleza na sasa
anaushikilia.
Analaumiwa na kushutumiwa na
wengi. Anakosolewa tena anabanwa na
wakubwa wa magharibi.
Hata hivyo, amepuuza hayo yote na
kuendelea na kile kinachotajwa na
wengi ‘ umwamba wa baadhi ya
viongozi wa Afrika kusalia madarakani
kwa kupindisha katiba zao’.
Tayari ameanza kuonja kile wengi
wanakiita joto la jiwe. Mkoloni wake
wa zamani, Ubelgiji ilikuwa nchi ya
kwanza kuuadhibu utawala wake.
Ubelgiji imesitisha baadhi ya misaada
ya maendeleo huku ukionya kuchukua
hatua zaidi katika siku za karibuni
iwapo ukandamizaji kwa makundi ya
wapinzani utaendelea.
Marekani imefuata mkondo. Rais
Barack Obama ametangaza kuing’oa
Burundi kutoka kwenye mikataba yake
ya kibiashara ya AGOA
inayoyawezesha mataifa ya Afrika
kuingiza bidhaa zao katika soko la nchi
hiyo bila ya kulipa kodi.
Mpango huo uliasisiwa wakati wa
utawala wa Rais Bill Clinton
anayetajwa ndiye aliyefufua upya
uhusiano wa karibu baina ya mataifa
ya Afrika na Marekani.
Rais Obama ambaye katika siku za hivi
karibuni amekuwa mstari wa mbele
kuwakosoa viongozi wa Afrika
wanaong’ang’ania kubakia
madarakani, alisema amechukua
hatua hiyo baada ya kushuhudia
kushuka kwa viwango vya demokrasia
katika taifa hilo.
Jinamizi la utamu wa madarakani bado
linaendelea kuzunguka. Rais Kagame
amefaulu kunyosha mstari tena kwa
wananchi wake.
Hata hivyo, wapinzani wake
wanalalamika kwa kile wanadai
kuandamwa na vitisho na wakati
mwingine kuwa hatarini kuuawa.
Ingawa amefaulu kushika ufunguo wa
kuendelea kusalia Ikulu kwa mkono
wa umma, lakini kivuli cha mwisho
wake bado kinatawaliwa na chenga.
Wengi wanaona kuwa, Rais Kagame
‘amejitengenezea’ maadui wengi
kuliko ilivyotarajiwa.
Hali kama hiyo inaanza kulinyemelea
taifa la Congo Brazzaville ambako Rais
Denis Sassou Nguesso ambaye wakati
fulani alipewa sifa kubwa kutokana
mchango wake wa kusaidia kutatua
migogoro ya Afrika. Inaelezwa kuwa
kwa sasa kiongozi huyo anageuka
kinyonga.
Ameanzisha mkakati wa kubadilisha
Katiba ya nchi hiyo ili awanie urais
katika muhula mwingine wa tatu.
Hata hivyo anakabiliwa na upinzani
mkali, lakini mwenyewe anasisitiza
kuwa lazima ajenda yake ipate
uungwaji mkono.
Japokuwa kila mwanasiasa huja na
mwonekano wake, lakini kwa walio
wengi wanahisi kuwa viongozi hao
wanajaribu kucheza kwenye utelezi
mkali huku wakiwa wamevalia suruali
yenye msumari pembeni.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni