Wananchi wa Tabata Dar es Salaam jana
wakiwa kwenye foleni ya kujiandikisha
kwenye Daftari la Kudumu la Wapigakura
kwa mfumo wa kieletroniki (BVR) katika
kituo kilichopo kwenye ofisi za Serikali ya
Mtaa wa Tabata Kisiwani. Picha na Salim
Shao
ADVERTISEMENT
Dar es Salaam. Mawakala
wanaoandikisha vitambulisho vya
wapigakura kwa kutumia mfumo wa
Biometric Voter Registration (BVR),
katika Kituo cha Shule ya Msingi
Umoja, wamegoma kuendelea na
uandikishaji kwa madai ya kutolipwa
posho.
Akizungumza kwa niaba ya mawakala
wenzake katika manispaa ya
Kinondoni, Yusufu Msigiti alisema
mkataba wao uliisha jana, lakini
walipewa malipo ya siku sita badala ya
kumi.
Alisema hata walipofuatilia
waliambiwa wanapaswa kulipwa na
manispaa au Serikali ya kata.
Hata hivyo, Ofisa Mtendaji wa Kata ya
Mabibo, Paul Ngunga alidai kuwa
alikaa kikao na mawakala hao
akawaeleza kuwa katika manispaa
hiyo, fedha iliyotoka ni ya siku sita tu,
hivyo waendelee kuwa na subira.
“Sehemu nyingine mawakala
wanaendelea na kazi, hawa ndiyo
hawajaelewa, wamegoma....
nimeshaleta mawakala wengine na
wanaendelea na kazi ya kuandikisha
wananchi,” alieleza Ngunga. Hata
hivyo, Msigiti alisema: “Hatujawahi
kulipwa na watu hao, lakini
tunashangaa mtendaji wa kata
anatuambia tuende huko, fedha
yenyewe wanayotulipa ni ndogo
tunafanya kazi ngumu kuanzia saa
moja asubuhi hadi saa 12 jioni.”
Msigiti alisema mtendaji huyo
aliwajibu vibaya baada ya kumhoji
kuhusu posho zao za siku nne ambazo
hawajalipwa badala yake aliwaambia
anayetaka kazi aendele na asiyetaka
aache.
Mawakala hao wamemtupia lawama
mtendaji huyo kwa majibu yake ilihali
wana malalamiko ya msingi.
Walisema hakukuwa na haja kwa
mtendaji huyo kuita polisi kwa lengo la
kuwazuia mawakala hao kudai haki
yao.
Wakala Peter Mnyika alisema polisi
walivyofika eneo hilo walimpiga
mwandishi wa habari aliyekuwa eneo
hilo na kumzuia kukusanya taarifa
zake.
“Alikuwa amevaa kitambulisho na
alijitambulisha baada ya kuona vurugu
zinazidi lakini askari mmoja wa kiume
alimkunja mwandishi huyo na baada
ya kuona waandishi wenzake wamefika
na kamera alikimbilia ofisi ya
mwalimu mkuu na hajatoka mpaka
sasa,” alieleza Mnyika.
Mwandishi aliyepigwa ambaye
hakutaka kutaja jina lake alisema
askari ndiyo wamekuwa wa kwanza
kumzuia kufanya kazi yake badala ya
kumpa ushirikiano.
Yusufu Kileme alikiri mtendaji wa kata
kutumia lugha mbaya wakati
mawakala wakidai haki yao.
Pia, alisema askari wanaofika eneo
hilo wanapaswa kuangalia anafanya
fujo ili wazuie, na siyo kuwa chanzo
cha vurugu.
Mwenyekiti wa kata hiyo, Saimoni
Ramo alisema askari walipofika
aliwasihi wasitumie nguvu kwa sababu
malalamiko ya vijana hao ni ya msingi.
“Askari walitakiwa kutumia busara na
siyo nguvu hili ni tukio dogo,
tunakoelekea ndiyo kukubwa zaidi.
Sasa kama wanafanya hivi, kwenye
Uchaguzi Mkuu siyo ndiyo
watatuvunjavunja,” alisema Rahino.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni