Jaji Damian Lubuva, Mwenyekiti NEC
Dar es Salaam. Tanzania inaelekea
kwenye Uchaguzi Mkuu, Oktoba 25,
mwaka huu. Baadhi ya wananchi hasa
vijana waliofikisha miaka 18 hivi
karibuni hawajawahi kushiriki kwenye
uchaguzi wowote na uchaguzi huu ni
wa kwanza kwao.
Vijana hawa na watu wengine,
wanahitaji kujifunza au kukumbushwa
juu ya mambo ya kufanya siku ya
uchaguzi ili kufanya zoezi la upigaji
kura kuwa lenye mafanikio na
kuepusha uvunjifu wa sheria
unaoweza kumweka mtu matatani.
Kwa bahati mbaya, elimu kwa
mpigakura haitolewi mara kwa mara
kwa wananchi mpaka nyakati za
uchaguzi. Hata wakati huo ukifika,
baadhi ya watu hasa wale wa hali ya
chini, hawafikiwi na elimu hiyo.
Elimu kwa mpiga kura bado
inahitajika ili kila mwananchi afahamu
haki na wajibu wake katika mchakato
mzima wa uchaguzi. Tume ya Taifa ya
Uchaguzi (Nec) ndiyo yenye jukumu la
kutoa elimu hiyo kwa kushirikiana na
wadau wengine.
Hata hivyo, zoezi hili linakabiliwa na
changamoto ya uhaba wa rasilimali za
kufanikisha utoaji wa elimu kwa
wapigakura. Vilevile, hakuna chombo
maalumu cha kuratibu na kusimamia
utoaji wa elimu ya uraia.
Mwenyekiti wa Nec, Jaji Damian
Lubuva anasema changamoto kubwa
wanayokabiliana nayo ni pamoja na
uhaba wa Asasi za kiraia zinazotoa
elimu kwa wapigakura na kuwafikia
wananchi wote nchi nzima.
Jaji Lubuva anasema Tume imejipanga
vizuri kuhakikisha kwamba elimu
inawafikia wapigakura nchi nzima.
Anasema watatumia vyombo vya
habari vikiwamo vinavyomilikiwa na
taasisi za dini ili kuwafikia wananchi
haraka zaidi.
Zingatia haya siku ya uchaguzi
Mkurugenzi wa uchaguzi – Nec,
Kailima Kombwey anafafanua mambo
muhimu ambayo mpigakura anatakiwa
kufanya siku ya uchaguzi bila kuathiri
masharti ya sheria za uchaguzi na
kanuni zake.
Wahi kituoni
Anasema jambo la kwanzana la msingi
ni kuwahi asubuhi katika kituo cha
kupigia kura. Kombey anasema
wananchi wanatakiwa kufika vituoni
kuanzia saa moja asubuhi wakiwa na
vitambulisho vyao vya kupigia kura.
Anasema kila mpigakura anatakiwa
kujua kituo atakachopigia kura na
kuhakiki kama jina lake lipo kwenye
orodha ya wapigakura kwenye kituo
husika.
Panga foleni
Kombey anabainisha kuwa watu
watapanga foleni kuingia chumba cha
kupigia kura na vituo vitafungwa
kuanzia saa 10 jioni. Anasema
watakaokuwa kwenye mstari baada ya
muda huo wataruhusiwa kuendelea
kupiga kura mpaka watakapomaliza.
“Tunasisitiza wananchi wajitokeze kwa
wingi ili wawachague viongozi wao.
Kupiga kura ni jambo la muhimu kwa
maendeleo ya Taifa letu.
Wasipojitokeza basi wasilaumu
kiongozi atakayechaguliwa na
wengine,” alisema Kombwey.
Mkurugenzi huyo anasema katika
uchaguzi wa mwaka 2010,
waliandikisha watu milioni 20 lakini
waliojitokeza kupiga kura walikuwa
chini ya milioni 10. Kwa hiyo,
anasisitiza zaidi kujitokeza kupiga
kura siku hiyo.
Usivae sare za chama
Jambo la pili, mpigakura asivae nguo
yenye nembo au alama yoyote ya
chama cha siasa kwenye kituo cha
kupigia kura. Kufanya hivyo ni kukiuka
taratibu za uchaguzi na mtuhumiwa
anaweza kushitakiwa kwa kuhujumu
mchakato wa upigaji kura.
Kombey anafananisha jambo hilo na
akufanya kampeni siku ya kupiga kura,
jambo ni kinyume na kanuni. Kwa
hiyo, fulana, kofia, bendera au kanga
au nguo yoyote inayovaliwa na chama
chochote haitakiwi kwenye eneo la
kupigia kura.
“Tunatoa muda wa kampeni ili
wanasiasa na vyama vyao wajinadi
kadri wanavyotaka lakini siku ya
uchaguzi siyo siku ya kufanya
kampeni, ni kinyume cha kanuni za
uchaguzi,” anasema mkurugenzi huyo.
Anaendelea kubainisha kuwa Tume
kupitia kifungu cha 124 (a) cha sheria
ya taifa ya uchaguzi ya mwaka 1985
ilianda maadili ya uchaguzi ambayo
yamefanyiwa mabadiliko madogo
mwaka huu na kukubaliwa na vyama
vyote.
Wahusika wakuu katika maadili haya
ni Tume ya Uchaguzi, Serikali,
wagombea na wanachama wote wa
vyama vya siasa. Kombwey anasema
wadau hawa kwa pamoja wana wajibu
wa kufanya uchaguzi huru na wa haki.
Usilete ushabiki
Jambo la tatu, wapigakura wasilete
ushabiki kwenye vituo vya kupigia
kura. Mambo ya ushabiki ni pamoja na
kuongelea matokeo ya uchaguzi kabla
hayajatangazwa na mamlaka husika
zilizokasimiwa jukumu hilo.
Mkurugenzi huyo anafafanua kwamba
jambo hilo linajenga hisia tofauti
miongoni mwa wapiga kura na
linaweza kusababisha vurugu endapo
matokeo yatakuwa kinyume chake.
Anabainisha kuwa kura ni siri ya
mpigakura mwenyewe.
“Sitarajii kuona watu wakitengeneza
makundi ya kujadili mwenendo wa
uchaguzi kwenye vituo. Hiyo ni sawa
na kampeni siku ya uchaguzi,
hatutaacha ufanyike kwa sababu
utaharibu mchakato wa uchaguzi,”
anasema.
Ukipiga kura nenda nyumbani
Jambo la nne, mwananchi akimaliza
kupiga kura aende nyumbani kusubiri
matokeo kutangazwa. Kuendelea
kukaa kwenye vituo vya kupigia kura
kunasababisha msongamano usio wa
lazima.
Kombwey anasema hakuna haja ya
kukaa kwenye vituo vya kupigia kura
kwa ajili ya kulinda kura kwa sababu
tayari mawakala wa vyama vya siasa
wapo kwa ajili ya kuangalia mwenendo
mzima wa uchaguzi.
“Ile dhana ya kutaka kulinda kura
zisiibiwe ndiyo inayosababisha vurugu
kwenye vituo. Hizo ni hisia tu, hakuna
wa kuiba kura kwa sababu kuna
mawakala wanaowakilisha vyama
vyao,” anasema.
Tume ina jukumu la kutangaza
matokeo
Anasema jukumu la kutangaza
matokeo ya urais ni la Tume ya
uchaguzi. Tume pia imekasimisha
jukumu la kutangaza matokeo ngazi ya
kata kwa msimamizi msaidizi wa kata
na ngazi ya jimbo kwa msimamizi wa
halmashauri.
Kombwey anasema kuna baadhi ya
watu wanatishia kutangaza matokeo
endapo Tume itachelewa kufanya
hivyo. Anasisitiza kuwa kufanya hivyo
ni kinyume cha utaratibu kwa sababu
hakuna mtu mwenye jukumu hilo zaidi
ya Nec.
Anasema Nec imejipanga kutangaza
matokeo ya urais ndani ya siku tatu
kwa sababu watatumia Mfumo wa
Kusimamia Matokeo (RMS) ambao
utawawezesha kupokea, kujumlisha na
kutangaza matokeo.
Licha ya kutakiwa kisheria kutangaza
matokeo hayo ndani ya siku saba, Nec
imebainisha kwamba mfumo huo
utasaidia kuongeza kasi ya ukusanyaji
wa matokeo kutoka sehemu mbalimbli
nchini.
Mabadiliko ya sheria
Jaji Lubuva anasema mabadiliko
makubwa ya sheria ya uchaguzi
yalifanyika mwaka 2010, mwaka huu
sheria hiyo haijafanyiwa marekebisho
isipokuwa kanuni za uchaguzi
zimerekebishwa ili kuleta ufanisi
katika uchaguzi ujao.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni