other blog

Jumanne, 22 Septemba 2015

Matajiri watano kuibeba Chadema Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema chama chake kina watu watano wenye uwezo wa kiuchumi


Mwenyekiti wa Chadema, Freeman
Mbowe (mwenye kipaza sauti) akiendesha
harambee ya kuchangia fedha kwa ajili ya
kampeni za chama hicho iliyofanyika Dar
es Salaam juzi. Picha na Said Khamis
Dar es Salaam. Mwenyekiti wa
Chadema, Freeman Mbowe amesema
chama chake kina watu watano wenye
uwezo wa kiuchumi wanaoweza
kukisaidia chama hicho kuendesha
shughuli zake za kampeni, ikiwa ni
siku 32 kabla ya wananchi kupiga kura
Oktoba 25.
Lakini mwenyekiti huyo wa Chadema
amesema watu hao hawataki
kutangazwa majina yao kutokana na
kuhofia kufuatiliwa na vyombo vya
dola, akisema kitendo hicho ni cha
kushangaza kwa nchi huru kama
Tanzania.
Chadema, ambayo inashirikiana na
NLD, CUF na NCCR Mageuzi chini ya
mwamvuli wa Umoja wa Katiba ya
Wananchi (Ukawa) iliandaa harambee
hiyo juzi kwenye ukumbi wa Mlimani
City kwa ajili ya kutafuta fedha za
kuchangia shughuli zao za kampeni
zinazoendelea kote nchini.
Katika hafla hiyo iliyohudhuriwa na
takriban watu 800, jumla ya Sh97
milioni zilikusanywa, ikiwa ni fedha
taslimu, michango kwa njia ya simu na
ahadi.
Baada ya kazi ya uchangishaji kuanza,
Mbowe alishika kipaza sauti na
kueleza michango mingine kutoka nje
ya ukumbi huo.
“Wakati tunaendelea na uchangiaji
hapa, nimepokea simu kutoka kwa
rafiki zangu watano wenye uwezo
mkubwa kiuchumi. Wameahidi
kuchangia harambee lakini wanaogopa
kujulikana kwa kuhofia mkono wa
serikali,” alisema mwenyekiti huyo.
“Inasikitisha Mtanzania mwenye uhuru
ndani ya Taifa lake anahofia kuchangia
safari ya mabadiliko kwa sababu ya
kuiogopa Serikali, wakati Serikali
iliyopo imejaa mafisadi wakubwa?
“Unaweza kuona hii ni Serikali ya
namna gani, lakini ningewaomba
niwatie moyo tu ndugu zangu wenye
nia ya mabadiliko, tuwe na ujasiri,
msiogope.”
Sheria ya Gharama za Uchaguzi,
ambayo mwaka huu imeweka kiwango
cha juu cha matumizi ya kila chama
kuwa Sh17 bilioni, inataka uwazi wa
vyanzo vya mapato na matumizi, lakini
ni nadra kwa wafanyabiashara kuweka
bayana michango yao kwa vyama vya
upinzani.
Chadema imekuwa ikinufaika na
michango ya fedha na mali kutoka kwa
mfanyabiashara maarufu nchini,
Mustapha Sabodo, ambaye amekuwa
akitangaza hadharani kila
anapokichangia chama hicho.
Alipoulizwa ni kiasi gani chama hicho
kimepanga kutumia kwenye uchaguzi,
Mbowe alisema ni vigumu kutaja.
“Uchaguzi ni dynamic
(unabadilikabadilika). Hesabu za siku
haziwezi kuwa sawa wakati wote. Kwa
mfano bango la kupinga bao la mkono,
inahitajika sana kwa wakati huu lakini
gharama inaweza kuwa nyingine
wakati wa kusambaza bango jingine,”
alisema Mbowe.
Mkurugenzi wa mipango na uchaguzi
wa CUF, Shaweji Mketo alisema kila
chama ndani ya umoja huo
kinajitegemea kwenye gharama za
wagombea wake kwa ngazi ya
majimbo na udiwani.
“Hakuna tathmini ya pamoja ya
Ukawa...taarifa za gharama kwa CUF
tutaziweka wazi baada ya kukamilisha
majumuisho ya taarifa zote kutoka
majimboni na ngazi ya madiwani,”
alisema Mketo.
Maoni ya wachambuzi
Mkuu wa Idara ya Sayansi ya Siasa wa
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM),
Dk Alexander Makulilo alisema hofu
kwa wafanyabiashara nchini
imekuwapo kwa muda mrefu.
Alisema ripoti ya Uchaguzi Mkuu wa
mwaka 2010 iliyoandaliwa na Timu ya
Waangalizi wa ndani wa uchaguzi
mkuu (Temco) inaonyesha TRA
kulalamikiwa na wafanyabiashara kwa
kuchunguza wafanyabiashara
waliokuwa hawaiungi mkono CCM.
Suala la matajiri hao kutotaka majina
yao kutajwa pia lilimgusa
mwanaharakati wa mtandao wa TGNP,
Gemma Akilimali, ambaye alisema
haoni sababu ya kuhofia kuchangia
kwa uwazi ili mradi ni wasafi katika
biashara zao.
“Sabodo ni mfanyabiashara mkubwa
tu na amekuwa akiwachangia
Chadema na CCM waziwazi bila
kuficha na hatujaona lolote likimtokea.
Kwa hivyo hofu zao zinaweza
kutujengea maswali katika uwazi wa
shughuli zao. Hofu iko kwa utayari
wao katika kuchimbuliwa shughuli zao
au vyanzo vya mapato yao.”
Awali kabla ya uchangiaji huo kuanza,
mgombea urais wa Chadema na
Ukawa, Edward Lowassa aliwataka
waalikwa kutoogopa kuchangia
harambee hiyo kwa hofu ya
kufuatiliwa na Mamlaka ya Mapato
(TRA).
“Nawaomba msiogope kuchangia, mtoe
tu kwani mabadiliko haya yanawahusu
wale wanaoyapenda na wasioyapenda.
Tunahitaji mabadiliko haya yafanikiwe
kwa kila hali,” alisema Lowassa,
ambaye aliihama CCM mwishoni mwa
mwezi Julai na kuungana na Chadema
kudai mabadiliko.
“Nawapongeza sana kwa juhudi za
maandalizi yaliyofanyika leo, na inatia
matumaini ya kufanikisha.”
Maombi ya uchangiaji
Akifungua harambee hiyo, Mbowe
alisema mikoa iliyosalia ni mingi kwa
hivyo bado wanategemea zaidi
michango ya wadau katika kufanikisha
kampeni.
Mbowe alisema muda uliobakia ni wa
“vita ya lala salama”, ambayo inahitaji
bajeti ya kutosha ili kufanikisha kufikia
wapiga kura wengi watakaoshiriki
uchaguzi huo.
“Ukichangia harambee hii hautakuwa
umemchangia Mbowe au Lowassa, bali
utakuwa umechangia ufanikishaji wa
kufikia ndoto ya mabadiliko. Utakuwa
umechangia ukombozi wa akina mama
na vijana wa Taifa la Tanzania,”
alisema Mbowe.
“Tangu kuanza kwa kampeni hizi,
Ukawa tumekuwa tukisaidiwa na
Watanzania mbalimbali wenye nafasi
zao, wapo waliotoa usafiri wa magari
ya kufanyia kampeni. Kwa hivyo
tunahitaji sana mchango wako katika
kipindi hiki.”
Chadema pamoja na Ukawa zimekuwa
zikipambana sambamba na CCM
kwenye kampeni za urais na ubunge
na matumizi yao makubwa
yanaonekana kuwa katika gharama za
safari za wagombea, matangazo ya
redio na televisheni, matangazo ya
moja kwa moja ya mikutano yao ya
kampeni, posho za mawakala na vifaa
kama mavazi, bendera, vipeperushi na
mabango.
Akizungumza kwenye hafla hiyo,
mwenyekiti mwenza wa Ukawa, James
Mbatia, ambaye ni pia ni mwenyekiti
wa NCCR-Mageuzi, aliwataka waalikwa
kuhakikisha wanashiriki kikamilifu
kuchangia harakati za mabadiliko ili
kufanikisha ndoto za kuwakomboa
Watanzania kutoka mikononi mwa
Serikali ya CCM.
Mwingine aliyezungumza na waalikwa
ni mgombea mwenza wa urais, Juma
Duni Haji, maarufu kwa jina la Babu
Duni, ambaye alikuwa kivutio kutokana
na vijembe na misemo anayotoa
wakati akiwa jukwani.
Duni alisema kutoa ni moyo na siyo
utajiri kwani wapo wenye fedha
nyingi, lakini hawana moyo wa utoaji.
Mzee wa Upako aibuka
Baada ya viongozi hao kuzungumza na
kuendesha harambee, Mchungaji
Anthony Lusekelo wa Kanisa la
Maombezi (GRC), Ubungo Kibangu,
alitaka watu kuwa tayari kukubali
matokeo yoyote kwa kuwa ushindi wa
Lowassa au mgombea wa CCM, Dk John
Magufuli utakuwa wa Watanzania
wote.
Baada ya kutoa kauli hiyo, waalikwa
walipiga kelele za kupinga kauli yake
lakini aliendelea kueleza msimamo
wake huku akiwatuliza.
“Tulia, tulia wewe unayepiga kelele,
siasa chafu hazifai na siasa siyo
kumchafua mtu,” alisema.
“Hakuna taasisi inayoweza kuzidi
nguvu ya umma, lakini niseme jambo
kwamba, kwa sasa tuna wagombea
wakubwa wawili ambao ni Dk
Magufuli na Lowassa. Yeyote
atakayeshinda itakuwa ni ushindi kwa
Watanzania, tusiweke nongwa. Mimi ni
kiongozi wa dini nisiyekuwa na itikadi
ya vyama, ninaishi na waislamu na
Wakristo, kwa hiyo ni sawa kwa yeyote
kati yao.”
Lusekelo alisema hana itikadi ya
chama chochote kile na Lowassa ni
rafiki yake kwamuda mrefu, lakini
endapo Dk Magufuli atashinda bado
itakuwa ni sawa kwake.
Mbowe alisema uchangiaji huo
unaendelea kufanyika kwa njia ya
akaunti maalumu za simu za mikononi
na kujaza fomu zilizoandaliwa kwa ajili
ya ahadi za wanachama ukumbini
hapo.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni