other blog

Jumatatu, 19 Oktoba 2015

POSTED BY ERASMI KIMARIO EAGLEFM Washauri mambo matano




Dar es Salaam. Zikiwa zimebakia siku
sita kabla ya kufanyika kwa Uchaguzi
Mkuu, Watanzania wameibua mambo
matano yanayoweza kuliepusha Taifa
na vurugu zinazoweza kutokea baada
ya uchaguzi.
Mambo hayo ni pamoja na uwazi wa
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC),
pande zinazohusika kuheshimu sheria,
wagombea kuwa wakweli kwa wafuasi
wao, kukaa pamoja kuweka mwafaka
wa kitaifa na NEC kuwa huru.
Mambo hayo yametajwa kukiwa na
mvutano kati ya vyombo vya dola na
viongozi wa vyama vya upinzani
kuhusu suala la wananchi kukaa mita
200 au kwenda majumbani baada ya
kupiga kura.
Tayari Rais Jakaya Kikwete
ameshaagiza vyombo vya dola
kuchukua hatua kali dhidi ya watu
watakaokaidi agizo la kuondoka kituoni
baada ya kupiga kura.
Mbali na mvutano huo, juzi wilayani
Tunduma mkoani Mbeya mfuasi
mmoja wa CCM alimuua kwa
kumchoma kisu mwanachama wa
Chadema, kabla ya yeye kuuawa pia.
Viongozi kukutana
Kutokana na hali hiyo, mhadhiri
kutoka Chuo Kikuu Huria cha Tanzania
(OUT), Emmanuel Mallya alishauri
viongozi wa vyama vyote
vinavyoshiriki uchaguzi huo wakutane
kujadiliana mambo ya kukubaliana
katika kipindi hiki kabla ya kufanyika
uchaguzi huo, Jumapili.
Mallya, ambaye ni Mkuu wa Idara ya
Sayansi ya Siasa chuoni hapo, alisema
kukutana kwa viongozi hao kutasaidia
kuwarejesha kwenye tafsiri ya
uchaguzi wa demokrasia badala ya
kuvutana kwa maslahi yao, hatua
inayoweza kuliathiri Taifa.
“Pili, uwazi wa NEC unahitajika zaidi
katika kipindi hiki, iwaeleze wagombea
kuweka mawakala waaminifu na
ijenge uhusiano mzuri na vyama,
taasisi za kiraia kwani dhamana ya
taifa ipo mikononi mwao na lazima
wanasiasa waongoze Taifa likiwa
salama na siyo walemavu,” alisema
Mallya.
Kufuata sheria
Profesa Gaudence Mpangalla wa Chuo
Kikuu cha Ruaha mkoani Iringa
alisema ili kuepuka vurugu ni
kuhakikisha sheria zinafuatwa.
Alisema ili kufuatwa sheria lazima
wanasiasa wajenge utamaduni wa
kuwa wakweli kwa wafuasi wao.
“Ushindani siyo vita wala uhasama
lakini inaonyesha kundi la vijana
limekosa uvumilivu na walitakiwa
kuelimishwa ukweli, watambue itikadi
zao haziwezi kuwa zaidi ya maslahi au
amani ya Taifa,” alisema Profesa
Mpangalla.
Uwazi wa NEC
Kwa upande wake, Profesa
Mohammed Bakari kutoka Idara ya
Sayansi ya Siasa, Chuo Kikuu cha Dar
es Salaam(UDSM), alitaja jambo
jingine linaloweza kunusuru amani ni
uwazi wakati wa shughuli za NEC.
Alifafanua kuwa licha ya vyombo vya
dola kujitahidi katika ulinzi, wafuasi
wa vyama vya siasa wanakosa imani
na NEC baada ya kuwazuia wasisubiri
matokeo ya uchaguzi mita 200 kutoka
vituoni, suala ambalo ni tofauti na
maelekezo ya sheria inayowataka
kukaa umbali wa mita 200 kutoka
kituoni.
“Mwaka 2010 walijikusanya kusubiri
kura na waliondoka wakiwa
wameridhika na matokeo lakini kwa
nini NEC izuie na kauli ya Rais
inatumika kama agizo la Amiri Jeshi
Mkuu, kwa hivyo dola lazima itekeleze
wakati kauli zake nyingine
zimeonyesha upendeleo kwa chama
chake, hii ni hatari sana,” alisema.
Vijana waepuke kutumika
Mwenyekiti wa Mtandao wa
Wanawake nchini, Profesa Ruth Meena
aliwataka vijana kuepuka kutolewa
kafara na wanasiasa wenye maslahi
yao ya kuelekea Ikulu.
“Burundi ilipochafuka kina mama,
watoto na vijana ndiyo walioanza
kuumia na machafuko lakini viongozi
walikuwa kwenye ulinzi mkali kwa
hivyo lazima vijana wajitambue itikadi
zao haziwezi kuwa zaidi ya maisha
yao,” alisema.
“Lakini pia wanasiasa wote lazima
wajiandae kupokea matokeo, hakuna
aliyeshinda au aliyeshindwa hadi sasa
na uchaguzi ni sawa na mchezo wa
soka kwani lazima kuna mmoja
atashindwa na mwingine kushinda.”
Vyombo vya habari kutenda haki
Katibu wa Jumuiya na Taasisi za
Kiislamu Tanzania, Sheikh Rajabu
Katimba alisema mbali na tahadhari
hiyo, Rais hatakiwi kutoa matamko
yanayokinzana na sheria zilizopo huku
vyombo vya habari vikitakiwa kutenda
haki.
“Kama ni haki ya kisheria kulinda kura
umbali wa mita 200 basi Rais Kikwete
anatakiwa kuheshimu hilo na
wananchi watamwelewa.”
“Lakini pia NEC inatakiwa
kuheshimiwa kwa sheria
inazosimamia, wafuasi wa vyama na
wagombea kujiepusha na kauli
zinazovunja sheria za uchaguzi na
mwisho kabisa vyombo vya habari
vitende haki katika kuripoti habari
zake,”alisema Katimba.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni