other blog

Jumatatu, 19 Oktoba 2015

POSTED BY VUMILIA NKYA A.K.A VEN DA CLASSIC....EAGLEFM... Magufuli: Asiyefanya kazi


Mgombea urais wa CCM, Dk John
Magufuli akihutubia mkutano wa kampeni
wilayani Misungwi, Mwanza jana. Picha na
Mpigapicha Wetu
Magu/Misungwi. Mgombea urais wa
CCM, Dk John Magufuli amewataka
wananchi kujipanga kufanya kazi kwa
sababu Serikali yake haitavumilia
watu wavivu.
Akihutubia mkutano wa kampeni
katika Uwanja wa Shule ya Msingi
Misungwi jana, Dk Magufuli alisema
hata vitabu vya dini vimeelekeza
kwamba asiyefanya kazi na asile, hivyo
wanaoahidi vitu vya bure
wanawadanganya Watanzania.
“Tujipange kufanya kazi, hata
maandiko ya vitabu vitakatifu
yanasema, asiyefanya kazi asile…
Misungwi nitaibeba kwa nguvu zangu
zote nikichaguliwa,” alisema.
Pia alisema nyumba za tembe ambazo
zinaahidiwa na wagombea wenzake
kwamba zitaondolewa ndani ya siku
100 ni uongo hivyo wasisikilizwe, bali
atakachofanya ni kuhakikisha bei ya
vifaa vya ujenzi inapungua na
ameanza na saruji.
Alisema anatambua kuwa wilaya hiyo
inakabiliwa na tatizo la maji na
kuwaahidi wananchi kulishughulikia
na wasimsumbue mbunge wao na
kwamba anapoahidi kutoa Sh50
milioni kila kijiji nchini watu
wanamshangaa lakini Serikali ina
fedha, nyingine zilikuwa zinatafunwa
na mafisadi.
“...Ndiyo maana baada ya kusikia
nimetangazwa mengine yakakimbia…
hivi sasa wanasema Serikali haijafanya
chochote wakati wengine wamezeekea
humu mpaka wakang’oka meno na
kuwekewa ya bandia, mbona
hawakuondoka muda wote?” alihoji Dk
Magufuli.
Mgombea huyo huku akichomeka
lugha ya Kisukuma kila mara, alisema
ujenzi wa barabara ya Usagara –
Kisema ukikamilika, malori yatakuwa
hayaruhusiwi kuingia katikati ya mjini
wa Mwanza. Aliahidi kufufua viwanda
vya kuchambua pamba ili kuleta
mabadiliko ya kweli.
Dk Magufuli aliahidi kufufua kilimo
cha pamba kwa kuhakikisha mkulima
anapata pembejeo na kunufaika na zao
hilo na kwamba, haiwezekani pamba
ilimwe Tanzania Ulaya wavae nguo
mpya halafu Watanzania waletewe
mitumba.
Hata hivyo, mgombea huyo akiendelea
kutoa ahadi sauti za wanawake
zilisikika zikimtaka kuzungumzia
samaki kazi ambayo ndiyo
wanayoitegemea kiuchumi, hivyo
akalazimika kutamka kuwa atafuta
ushuru unaoonekana kuwa kero.
“Nitafufua Chuo cha Kilimo Ukiriguru
na kutumia wataalamu wake
kuboresha kilimo cha pamba,”
alisema.
Mgombea ubunge Jimbo la Misungwi,
Charles Kitwanga alisema kuna sifa ya
Dk Magufuli ambayo haijatajwa nayo
ni ubunifu, kwani alianzisha mfuko wa
kujenga barabara kwa fedha za ndani
hali iliyowashangaza wafadhili.
“Hizi barabara tunazotaja kama siyo
yeye zisingekuwapo, mnakumbuka
wafadhili walikuwa wanakataa
kutukopesha, akaanzisha mfuko wa
kujenga barabara mpaka wafadhili
wanauliza fedha zitakapopatikana,
akawaambia tunazo,” alisema.
Kitwanga alimwomba mgombea huyo
kuwajengea hospitali ya wilaya na
kiwanda cha kusindika nyanya, zao
linalolimwa kwa wingi.
Akiwa Magu, Dk Magufuli alisema
endapo atachaguliwa, ataubadilisha
mji huo kwa kutatua kero sugu ya maji
na kujenga barabara zinazozunguka
mji huo. Alisema atatumia uwezo wake
wote kuhakikisha kilimo cha pamba
kinakuwa bora ili bei ya zao hilo
ipande na kuwanufaisha wakulima.
Akihutubia umati wa watu kwenye
Viwanja vya Sabasaba jana, Dk
Magufuli alisema: “Natambua kwamba
Magu shida yenu kubwa ni maji,
mmekuwa mkitaabika kwa muda
mrefu, huku Ziwa Victoria likiwa
limewazunguka.
“Kwa kutambua kwamba maji ni
muhimu kwa binadamu, hapa Magu
lazima mpate maji na tayari Kampuni
ya Cowi inafanya upembuzi yakinifu
kuhakikisha maji yanafika,
wakikamilisha tu suala la maji kufika
Magu niacheni mimi...”
Dk Magufuli alisema anataka kuona
Magu inabadilika na kwamba
ameahidi kujenga barabara
zinazozunguka mji huo na kuunganisha
wilaya jirani.
Alisema amezaliwa na kulima pamba
pamoja na kufuga, hivyo ni mtoto wa
mkulima na mfugaji na kwamba
atatumia uzoefu wake kuhakikisha bei
ya pamba inakuwa juu. “Nafahamu
kwamba bei ya pamba kwa sasa
imeshuka, lakini mimi ni mtoto wa
mkulima na mfugaji, pamba
naifahamu vizuri, nataka tutengeneze
mazingira mazuri kwa wakulima wa
pamba ili iwe bora,” alisema Dk
Magufuli.
Aliwataka wakazi wa mji huo, kula
fedha za watu wanaowahonga ili
wawachague, akisema hizo ni fedha
zao ambazo walizichuma kwa kutumia
ufisadi.
“Nyie mkipewa fedha kuleni, kwani
kula ni kwa mafisadi kulala kwa
Magufuli,” alisema na kuongeza kuwa
akichaguliwa, atakuwa rais wa watu
wote, kwa kuwa maendeleo hayana
chama.
Aliahidi kufuta ushuru ambao
umekuwa ukiwasumbua
wafanyabiashara ndogondogo
sambamba na kupunguza kodi za vifaa
vya ujenzi ili bei ya vifaa hivyo
ipungue na kuwawezesha wananchi
kununua na kujenga nyumba bora.
Imeandikwa na Aidan Mhando, Midraji
Ibrahim na Twalad Salum

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni