other blog

Jumatatu, 19 Oktoba 2015

POSTED BY PINDA ..EAGLEFM

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda
Dar es Salaam. Waziri Mkuu Mizengo
Pinda, jana alitumia Ibada ya Shukrani
iliyofanyika katika Parokia ya
Hananasifu, Jimbo Kuu Katoliki la Dar
es Salaam, kumshukuru Mungu kwa
kumwezesha kulitumikia Taifa kwa
zaidi ya miaka 15 na kuwaomba
Watanzania wamsamehe kwa
matamshi aliyoyatoa akiwa kiongozi,
huenda yaliwakwaza baadhi yao.
Pinda ambaye amekuwa Waziri Mkuu
kwa miaka minane na miezi tisa,
Waziri kwa miaka miwili na nusu na
Naibu Waziri kwa miaka mitano,
alisema anasikia fahari kumaliza
uongozi wake kwa furaha na amani.
Moja ya kauli tata zilizowahi kutolewa
na kiongozi huyo iliyozua sintofahamu
ni ile ya Juni 29, 2013 katika ukumbi
wa Bunge mjini Dodoma alipoviagiza
vyombo vya dola kuwashughulikia kwa
kuwapiga wale watakaokataa kutii
amri wakati wakifanya vitendo vya
uvunjifu wa amani.
Kauli nyingine tata ni ile ya mwaka
2009 baada ya kuwaeleza wanaoua
watu wenye ulemavu wa ngozi
(albino) pamoja na vikongwe hawana
budi kuuawa kwa kuwa wakisubiri
mahakama kuwahukumu, watakuwa
wanakosea.
“Katika ibada hii ya shukrani,
nimemuomba Mungu anisamehe kwa
matamshi niliyoyatoa nikiwa kiongozi
yanaweza kuwa yaliwaudhi watu bila
mimi kujua.
“Uwaziri Mkuu ni kazi ngumu yenye
changamoto nyingi. Nitakuwa mtu wa
ajabu nisipomshukuru Mungu kwa
uongozi wake katika kipindi chote
hicho tangu nikiwa naibu waziri hadi
kuteuliwa kuwa Waziri Mkuu,”
alisema.
Pinda alisema katika utumishi wake
kwa umma amejifunza mambo mengi
lakini kikubwa zaidi ni kujua jinsi ya
kuishi na watu.
Katika hatua nyingine, Abate Thadei
Mhagama wa Abasia ya Hanga,
aliwataka waumini nchini wazidishe
maombi kwa kufunga na kuomba kwa
siku sita zilizobaki kabla ya kufanyika
kwa Uchaguzi Mkuu.
“Ninawaomba waumini wote tuzidishe
sala ili nchi iendelee kuwa na amani
na upendo, tumwombe Mungu pia
atuwezeshe kupata viongozi
aliowandaa kwa yeye kwa maana ya
rais, wabunge na madiwani,” alisema
Mhagama.
Alisema uchaguzi wa mwaka huu ni wa
aina yake kwani demokrasia imekuwa
miongoni mwa Watanzania.
“Sote ni mashahidi, tumeona kwenye
mikutano kila mgombea akija sote
tunajaa huko. Hii ni kwa sababu
hatujui yupi ni yupi, ndiyo maana
nasisitiza kuwa tumuombe Mungu
atuletee yule ambaye amemuandaa
yeye,” alisisitiza.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya
Baraza la Walei katika parokia hiyo,
Arbogasti Warioba alisema:
“Sote tunatambua kuwa kazi
aliyoifanya Waziri Mkuu Pinda ilikuwa
ngumu, misafara ilikuwa ni mingi na
wakati mwingine ilikuwa ya mwendo
mkali, lakini Mungu alimtetea na
kumlinda hadi leo yuko salama.
Tunakushukuru pia kwa ushirikiano
ulioendelea kutuonyesha wakati ukiwa
madarakani na tunakuombea uendelee
kuwa na ucha Mungu katika maisha
yako ya uraiani.”

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni