other blog

Jumatatu, 27 Julai 2015

Hatimaye dar foleni ipo palepale pamoja na kuongezwa kwa vbr ....


Dar es Salaam. Wakati mashine za
Biometric Voters Registration (BVR)
zikiongezwa kulingana na mahitaji,
zogo limezuka kwenye Kituo cha Mtaa
wa Saranga, Kimara baada ya
wananchi waliojiorodhesha kufikia
10,000 huku kukiwa na mashine tatu.
Zogo hilo lilitokana na baadhi ya
wananchi kufika kwenye kituo hicho
alfajiri jana, wakiamini wamewahi,
lakini walishangaa waandikishaji
kuanza kuwaita waliowawekwa viporo
tangu juzi. Baadhi ya wananchi
walisikika wakitishia kumpiga mmoja
wa wasimamizi wa kazi hiyo Sada
Mbonde, aliyepewa jukumu la
kuwapanga watu foleni.
Mbonde alisema wananchi hao
wanamuweka katika wakati mgumu
kwa kuwa waliosalia juzi
waliorodheshwa kwenye karatasi na
kuahidiwa kukamilishiwa taratibu za
kupata vitambulisho vyao jana.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Saranga,
Godwin Muro aliiomba Tume ya Taifa
ya Uchaguzi (NEC), kuongeza mashine
ili wananchi wengi waandikishwe kwa
kuwa wako zaidi ya 10,000.
Wakati huohuo; kutokana kugoma
kufanya kazi mashine za BVR,
wananchi wa Kata ya Kimara, Kituo
cha Shule ya Chekecheke ya Mtakatifu
Thomas walitaka kuwafukuza
waandikishaji baada ya kugundua
kuwa changamoto hiyo taarifa
zilikuwa hazifiki kwa uongozi husika ili
kutatua.
Wananchi hao ambao walifika kituoni
hapo alfajiri, walisubiri kwa muda bila
mafanikio na ilipotimu saa 8:00
mchana walimtaarifu mwenyekiti wao,
Rafael Mlay suala hilo.
“Nimezungumza na mkurugenzi na
ameniambia kuwa hana taarifa kama
kituo hiki kina mashine moja, anajua
kuwa zipo tatu, hivyo ameagiza
nyingine mbili zije mara moja. Zipo
njiani zinakuja, nawashauri
muendelee kusubiri ili mambo yaende
sawa,” alisema Mlay.
Baada ya kauli hiyo ya mwenyekiti,
wananchi hao waliwataka maofisa
waliotumwa na NEC waondoke kwa
madai kuwa wanawafanyia hujuma
kwa kuwa wengi wao ni wafuasi wa
chama pinzani.
Ilipotimu saa 10:30 jioni, Mlay
alilijulisha gazeti hili kwa simu kuwa
mashine moja imeongezwa na ile ya
mwanzo imetengenezwa hivyo
uandikishaji unaendelea kama
kawaida.
Hata hivyo, katika maeneo mengine
uandikishaji umeonyesha mafanikio
baada ya kuongezwa kwa mashine za
uandikishaji na kupunguza
msongamano wa watu.
Katika Kituo cha Shule ya Msingi
Segerea, mashine moja iliongezwa na
kufanya kituo hicho kuwa na mashine
mbili.
ADVERTISEMENT
Hali ilikuwa tofauti katika Kituo cha
Ofisi ya Mtendaji wa Mtaa wa
Migombani kwa kuwa hakukuwa na
foleni.
Mkazi wa Mtaa wa Migombani, Kata ya
Segerea, Amina Ramadhan alisema
alifika kituoni saa mbili asubuhi, lakini
hadi saa nne asubuhi alipata
kitambulisho chake.
Katika vituo vya Shule ya Msingi
Jangwani na Kunduchi mashine
ziliongezwa kutokana na mwitikio wa
wananchi.
Ofisa Mtendaji wa mtaa wa huo, Said
Kikuwi alisema mwanzoni walikuwa na
mashine moja kwa kila kituo, lakini
waliongezewa nyingine mbili kutokana
na wingi wa watu.
Katika Kituo cha Salasala, Mbezi Beach
pia uandikishaji ulifanyika vyema
kutokana na kuongezwa mashine.
Foleni haikuwa kubwa kutokana na
utaratibu wa kuitwa majina kwa
namba.
Ofisa Mtendaji wa Mtaa wa Salasala,
Abdallah Mbupi alisema wakati
uandikishaji unaanza walikuwa na
mashine saba, lakini hadi jana
walikuwa na mashine tisa.
Mwandishi msaidizi katika Kituo cha
Zahanati ya Kawe, Jaston William
alisema wananchi pia wamekuwa
sehemu ya changamoto kubwa katika
utendaji wa kazi hiyo.
“Watu wanapeana namba mtaani
halafu wakija hapa asubuhi tukianza
kuwaandikisha wale tuliowakuta ni
ugomvi. Sasa tumeweka utaratibu wa
kutoa namba kwa watu 100 ambao
tunawaandikisha kwa siku moja
wanaobaki tunawaandika majina
wanaendelea na shughuli zao kwa
sababu tuna mashine moja,” alisema.
Mwandikishaji msaidizi katika Mtaa wa
Changanyikeni, Kituo cha Chuo cha
Takwimu, Vincent Emmanuel alisema
kazi inaendelea vizuri, lakini
changamoto kubwa ni nguvukazi.
“Kama kila kituo kingekuwa na fundi
wa hizi mashine ingekuwa vizuri. Kwa
sasa kila kata ina fundi mmoja, hivyo
ni rahisi kukuta muda mfupi baada ya
kuondoka katika kituo husika tatizo
jingine likajitokeza hivyo kuchukua
muda mrefu kurekebishwa au
kumsubiri fundi,” alisema.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni