other blog

Jumamosi, 25 Julai 2015

Serikali imesikia ujumbe huu wa Ukimwi?

MWISHONI mwa wiki iliyopita, mkutano mkubwa wa wanasayansi na mashirika makubwa ya kimataifa yanayoshughulika na masuala ya Ukimwi ulifanyika jijini Vancouver, Canada na kutoka na ripoti yenye maana kubwa kwa nchi kama yetu.Watafiti na wanasayansi hao walitoa taarifa kuhusu ugunduzi mpya unaoonyesha kwamba mtu aliyebainika kuwa na virusi vya Ukimwi (VVU) ataishi maisha marefu zaidi endapo atapewa dawa za kupunguza makali (ARV) mapema kabla ya kuanza kuonyesha dalili za Ukimwi.Ugunduzi huu unaelezwa kuwa muhimu zaidi katika tafiti za Ukimwi hapa duniani katika kipindicha miaka 20 iliyopita, baada ya ule wa mwaka 1996 wakati mkutano kama huo uliofanyika Canada, ulipokuja na utafiti wa waathirika kutumia ARV.Kabla ya utafiti huo, mtu kukutwa na VVU ilikuwa sawa na kuandikiwakifo lakini sasa baada ya kupatikana kwa ARV, waathirika wanaishi maisha marefu kwa kadriwatakavyoweza kufuata masharti.Tunadhani kuwa sasa serikali na wadau wengine wanapaswa kujielekeza katika kampeni muhimu ya kuwataka watu wapimwe na kubaini hali zao za maambukizi kwa vile hilo litaokoa maisha ya wengi.Ilikuwa imezoeleka, huko nyuma, kuwa mtu anayetakiwa kutumia ARV ni yule ambaye ameatha kuonyesha dalili za kuathirika na maambukizi ya VVU lakini utafiti huu mpya unaonyesha kuwa hali nitofauti.Kama walivyosema watafiti na wanasayansi kupitia mkutano huo wa Canada, ni jukumu la serikali sasa kuhakikisha kuwa watu wengi zaidi wanapima na kupewa dawa za kupunguza makali mapema kabla hawajaanza kuumwa.Si siri kuwa Tanzania ni mojawapo ya nchi zilizoathiriwa na ugonjwa huu hapa duniani ingawa takwimu za karibuni zinaonyesha kupungua kwa kiwango cha maambukizi.Kiwango cha maambukizi cha sasa cha asilimia 5.1 kinaonyesha taifa letu bado halijaondokana kabisa na madhila ya ugonjwa huu. Kinachotakiwa ni kuhakikisha wale wanaopata maambukizi sasa, wapate dawa mapema ili waweze kuishi maisha marefu zaidi.Kuna faida kuu mbili za kupima mapema. Mosi kunaondoa uwezekano wa kuenea kwa maambukizi kwa vile waathirika watakuwa wanajijua na hivyo kuweza kujikinga na kuwakinga wenzao na pia wataishi maisha marefu zaidi.Hili linawezekana kama kila mhusika atachukua hatua.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni