other blog

Alhamisi, 20 Agosti 2015

CCM yazindua ilani yake,.. na kusema ushindi ni lazima


Mgombea urais wa CCM, Dk John
Magufuli na mgombea mwenza, Samia
Saluhu Hassan
Dar es Salaam. Hatimaye Chama cha
Mapinduzi (CCM) kimeipua Ilani yake
ya Uchaguzi kwa mwaka 2015-2020,
ikitaja mambo makuu manne ya
kushughulkikia katika miaka mitano
ijayo, ambayo ni kupambana na
umaskini, ajira kwa vijana, ulinzi na
usalama na kupambana na rushwa
kwa kuanzisha mahakama maalumu ya
makosa hayo.
Ilani hiyo, iliyoandaliwa na makada
wake 32 wakiongozwa na Stephen
Wasira, imeanisha jinsi chama hicho
kikongwe kilivyotekeleza baadhi ya
ahadi zake katika ilani ya mwaka
2010-2015 na kutaja ahadi mpya
zikiwamo zinazohusu ujenzi wa
miundombinu, kukuza uchumi,
viwanda, nishati, kilimo, sanaa na
michezo pamoja na kuimarisha ulinzi
na usalama.
“Ilani hii ni tamko maalumu kwa
wapigakura kuhusu nia ya CCM ya
kuendelea kushika dola na
kuwaongoza Watanzania kwa njia ya
kidemokrasia na hasa kuendelea
kudumisha amani, umoja wa kitaifa,
usawa, ustawi wa wananchi, Muungano
wa Tanganyika na Zanzibar na
Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar kwa
kipindi kingine cha miaka mitano,”
inasema ilani hiyo.
Kukamilika kwa ilani hiyo sasa
kutamuweka huru mgombea urais wa
CCM, Dk John Magufuli ambaye
amekuwa akisita kumwaga sera
kwenye mikutano ya hadhara kwa
hofu ya kukiuka Sheria ya Uchaguzi na
pia kutokuwapo kwa ilani hiyo.
Mkutano Mkuu wa CCM ulikuwa
upitishe ilani hiyo Julai 12 mjini
Dodoma, lakini mwenyekiti wa chama
hicho, Jakaya Kikwete akaeleza kuwa
ilikuwa katika hatua za mwisho za
uhariri na kuomba chombo hicho
kiridhie kazi hiyo kukamilishwa na
Halmashauri Kuu.
Kwa mujibu wa ilani hiyo yenye
kurasa 236, katika miaka mitano ijayo
CCM itazielekeza Serikali zake za
Muungano na Zanzibar kuboresha
maisha ya wananchi wote na hususan
vijijini, kwa kuchukua hatua
mbalimbali ilizoziainisha, zikiwamo
kukuza kilimo, miundombinu,
viwanda, ajira na kupambana na
rushwa.
Katika suala la rushwa, ilani hiyo
imetaja mkakati wa mmoja wa makada
walioomba kuwania urais kwa tiketi ya
chama hicho, Frederick Sumaye wa
kuanzisha mahakama maalumu ya
kushughulikia matatizo ya rushwa.
Ilani hiyo inaeleza kuwa CCM
itaimarisha “vyombo na taasisi
zinazohusika katika kuzuia na
kupambana na rushwa, ikiwa ni
pamoja na kuanzisha mahakama
maalumu kwa ajili ya makosa ya
rushwa na uhujumu uchumi”.
Mkakati huo umekuja wakati chama
hicho kikikabiliwa na tuhuma za
rushwa, hasa katika mchakato wa
uchaguzi huku makada wake
wakihusika katika kashfa zilizotikisa
Taifa, hasa ya uchotwaji fedha kwenye
Akaunti ya Tegeta Escrow
iliyosababisha mawaziri wawili
kuachia ngazi, sambamba na
Mwanasheria Mkuu, wabunge na
baadhi ya watendaji waandamizi wa
Serikali.
CCM inaeleza katika ilani hiyo kuwa
imedhamiria kukuza uchumi kwa
miaka mitano ijayo kwa wastani wa
asilimia nane au zaidi, kuinua ustawi
wa Watanzania kwa kuongeza mapato
ya wananchi kufikia kiwango cha
wastani wa nchi ya uchumi wa kati,
hivyo kuongeza fursa za ajira na
kupunguza umaskini.
Ahadi nyingine katika kukuza uchumi
ni pamoja na kudhibiti mfumuko wa
bei uendelee kubaki kwenye tarakimu
moja, kudhibiti nakisi ya bajeti ili
iendelee kushuka na kufikia kiwango
kisichozidi asilimia tatu ya Pato la
Taifa, pamoja na mambo mengine,
Tanzania iendelee kupunguza
gharama za kukopa kwa ajili ya
maendeleo ya nchi.
Katika miundombinu, CCM
imeendeleza ahadi za kujenga
barabara, madaraja, vivuko, viwanja
vya ndege, nyumba na majengo ya
Serikali ili kuongeza kasi ya
maendeleo ya kiuchumi na huduma za
jamii.
Hata hivyo, msisitizo wa ujenzi wa
barabara umewekwa zaidi katika zile
zinazounganisha Tanzania na nchi
jirani, mikoa, na barabara
zinazokwenda kwenye maeneo yenye
fursa za kiuchumi kama Mchuchuma
na Liganga na kujenga madaraja
mapya ya Selander jijini hapa na
Wami Chini la mkoani Pwani.
CCM imekusudia kuhamasisha kilimo
kupitia kaulimbiu ya Kilimo Kwanza,
kwa kuwawezesha wakulima kupata
mafunzo ya kilimo cha kisasa,
pembejeo, zana za kisasa na
wataalamu wa ugani pamoja na mbinu
za kuyafikia masoko ya uhakika ya
mazao yao.
CCM inakusudia kuongeza kasi ya
kupima ardhi na kuwapatia hatimiliki
za kimila wananchi, ambazo
watazitumia kama dhamana ya
kuwawezesha kupata mikopo ya
kuendeleza shughuli mbalimbali za
kilimo, ufugaji na uvuvi.
“Kuendeleza na kuimarisha huduma
za kijamii ikiwamo elimu, afya, maji,
umeme na ujenzi wa nyumba bora
pamoja na kuongeza kasi ya
kurasimisha biashara kwa kuwapatia
wafanyabiashara wadogo maeneo ya
kufanyia biashara, leseni na fursa za
kupata mikopo yenye masharti nafuu,”
ilani hiyo inaeleza.
“Kuanza na kukamilisha ujenzi wa
viwanja vya ndege vya Shinyanga, na
Sumbawanga kwa kukarabati
barabara za kutua na kuruka ndege,
kujenga na kukamilisha awamu ya pili
viwanja vya Tabora na Kigoma na
kuanza ujenzi wa kiwanja cha Ndege
cha Msalato kwa kiwango cha
kimataifa,” inasema ilani hiyo.
Katika sekta ya afya, CCM imeahidi
masuala mbalimbali ikiwamo kujenga
hospitali tatu za rufaa kwa Kanda za
Kusini, Kati na Magharibi na
kuendelea kuimarisha zilizopo.
Iwapo itapatiwa ridhaa ya kushika
dola, CCM imepanga kudahili
wanafunzi 15,000 katika vyuo vya afya
ifikapo 2020 kama jitihada kutosheleza
mahitaji ya rasilimali watu na kuajiri
wataalamu zaidi wa afya kutoka ndani
na nje ya nchi kuboresha huduma za
afya.
Ahadi nyingine ni kuimarisha
upatikanaji wa dawa, huduma za
mama na mtoto, kuimarisha huduma
za matibabu ikiwamo kununua
mashine za mionzi kwa ajili ya
saratani na kuweka utaratibu wa
wananchi kupata Bima ya Afya.
Kwa kutambua umuhimu wa ukuaji wa
sekta ya mawasiliano, sayansi na
teknolojia, CCM imeahidi kutenga kila
mwaka kiasi kisichopungua asilimia
moja ya pato ghafi la Taifa (GDP), kwa
ajili ya utafiti, maendeleo na
maonyesho.
Pia, kuwalinda watumiaji wa simu za
mikononi dhidi ya uhalifu wa
mitandaoni na kuongeza watumiaji wa
intaneti kutoka milioni tisa mwaka huu
hadi kufikia milioni 20 mwaka 2020.
Wakati baadhi ya wakosoaji wa
masuala ya elimu wakieleza kuwa
ubora wa elimu unapungua, CCM
imekusudia kuhakikisha uandikishwaji
wa rika lengwa la wanafunzi wa kidato
cha kwanza unaongezeka kutoka
asilimia 60 mwaka 2015 hadi asilimia
80 mwaka 2020... “Ufaulu wa mtihani
wa kidato cha nne utaongezeka kutoka
wastani wa asilimia 69.8 mwaka 2015
hadi asilimia 90.0 mwaka 2020 na
ufaulu wa daraja l hadi lll kutoa
wastani wa asilimia 30.8 hadi asilimia
50.0.”

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni