other blog

Jumatano, 26 Agosti 2015

Je unakumbuka haya mazuri ya lowassa... yaone hapa

Lowassa aendelea kuumbua vigogo
Ingawa Wahenga wana msemo
usemao mgeni njoo mwenyeji
apone kwa mabosi wa mkoa wa
Kigoma hali imekuwa tofauti
baada ya mgeni wao, Waziri
Mkuu Bwana Edward Lowassa
kuwaonjesha joto ya jiwe
hadharani.
Miongoni mwa walioonja
shubiri ya Waziri Lowassa
ni Mkuu wa Wilaya ya
Kigoma, Bw. John Mongella
ambaye bila kutarajia
alijikuta akikatizwa kusoma
ripoti yake yenye kurasa
zaidi ya 10 wakati ndiyo
kwanza amefika ukurasa wa
tatu.
Ripoti hiyo ilianza
kumchafua Waziri Mkuu pale
Mkuu huyo wa Wilaya
aliposema kuwa chanzo cha
kuzorota kwa kilimo cha
kahawa ni ukosefu wa
wataalam wa zao hilo.
Bw. Lowassa akasema hayo ni
mambo ya zamani asiyotaka
kuyasikia katika ziara yake
na badala yake anahitaji
kuona wakuu hao wa wilaya
wakionyesha kwa vitendo
uelewa wao baada ya kupigwa
msasa wa nguvu na Rais
Kikwete kwenye semina
elekezi iliyomalizika hivi
karibuni huko Arusha.
’’John huna taarifa,
afadhali twende kwenye
ziara’’, akasema Bw.
Lowassa na kuinuka
kuendelea na ziara.
Bosi mwingine aliyekumbwa
na kasheshe hilo ni Mkuu wa
wilaya ya Kibondo Luteni
Kanari John Mzurikwao
ambaye naye aliambiwa
ripoti yake ni mbovu.
Waziri Mkuu akazidi
kumuumbua mkuu huyo wa
wilaya kwa kusema kuwa
anashangazwa na utendaji
wake wa kazi kwa vile ni
tofauti kabisa na jinsi
anavyomfahamu.
Akasema inaonekana wakuu
hao wa wilaya hawakuambulia
kitu katika semina elekezi
iliyoendeshwa na Rais
Kikwete hivi karibuni
katika hoteli ya Ngurdoto
iliyopo nje kidogo ya Jiji
la Arusha.
’’Inaonyesha kuwa semina
ile haikueleweka wala
hotuba ya Rais aliyoitoa
mwishoni mwa mwezi uliopita
haikusikilizwa, ndio maana
mambo haya yanajitokeza’’,
akasema Bw. Lowassa.
Kana kwamba hiyo haitoshi,
Lowassa pia akamuibukia
Katibu Tawala wa wilaya ya
Kigoma, Bw. Martin
Mgongolwa na wakurugenzi wa
wilaya hiyo kwa kushindwa
kumsaidia mkuu wa wilaya na
badala yake wakamuandalia
hotuba iliyopitwa na
wakati.
Akasema Mkuu wa wilaya hiyo
bado ni mgeni na anahitaji
msaada wa viongozi wengine
wa wilaya ambao wana uzoefu
na maeneo yao.
’’Mnashindwa kuwasaidia
vijana hawa na mnataka sisi
tuwashambulie bure’’,
akacharuka Bw. Lowassa.
Waziri Mkuu yuko mkoani
Kigoma kwa ziara ya siku
tano akikagua miradi
mbalimbali ya maendeleo.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni